Thursday, 4 June 2015

Ohoooooo.......! NEY NA HAWA TEEENA ??? source GP




HII sasa kali! Wasanii wa sinema ndani ya Bongo Movies, Fatuma Ayubu `Bozi’ na Brenda Marembeka `Kunguru’ wametoa aibu ya mwaka baada ya kupigana kwenye baa tena mchana kweupe kwa kile kilichodaiwa walikuwa wakigombea mabwana ambao ni mastaa  wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ huku Kasim Yusuf `Young D’ naye akitajwa.

 
Wasanii wa sinema ndani ya Bongo Movies, Fatuma Ayubu `Bozi’ na Brenda Marembeka `Kunguru’ wakiamuliziwa baada ya kuzichapa.
 
Sekeseke hilo la aina yake lilijiri Jumatatu iliyopita kwenye Baa ya Mawela iliyopo Sinza jijini Dar ambapo kwa mujibu wa shuhuda mmoja wa tukio hilo, Bozi alitangulia kufika mahali hapo na kuagiza kinywaji.
 
WALIFIKA TOFAUTI
“Baada ya muda yule mwenzake (Kunguru) akafika na kuanza kumrushia vijembe mwenzake kisha kummwagia kinywaji chake na kumvua wigi alilokuwa amevaa.“Yaani hawa wasanii siyo siri wanaidhalilisha tasnia. Yule mwenzake alipofika tu, bila hata salamu akaanza kumtupia maneno makali mwenzake huku akimtuhumu kwa nini alitembea na bwana wa rafiki yake ambaye ni Nay wa Mitego kisha akaanza  kumkunja.
 
WAUMBUANA

“Yule mwingine (Bozi) akapamba moto na yeye, akasimama na kumuwakia mwenzake akimwambia  alitembea na bwana wake ambaye ni Yuong D. Yaani wamesababisha watu kujazana na kusitisha shughuli zao,” alisema shuhuda huyo.

MENEJA APATA WAKATI MGUMU
Wakati maparazi wanafika eneo la tukio walimkuta mtu mmoja aliyetambulishwa kuwa ni meneja wa baa hiyo akiwa katikati kuwaamua wasanii hao na kuambiwa waondoke.

 
Wakitupiana maneno baada ya kuamuliziwa.
 
WAHUDUMU PIA WANENA
Mbali na meneja kuwataka waondoke, wahudumu wa baa hiyo maarufu nao walionekana kutofurahishwa na kitendo cha wasanii hao kuzichapa kwenye baa hiyo kiasi cha kuwabughudhi wateja. Waliwatolea matusi mazito ambayo hayaandikiki gazetini huku wakiwaambia siku wakiziona sura zao kwenye baa hiyo wataishia polisi.

WENYEWE SASA
Baadaye kwa njia ya simu, mapaparazi wetu waliwatafuta wasanii hao, kila mmoja kwa wakati wake na kuwahoji juu ya ugomvi wao uliosababisha kujaza watu baa ambapo kila mmoja alimtupia lawama mwenzake kwa usaliti.

BOZI
“Yule Kunguru kwa kipindi kirefu hatujaonana na wala hatuongei. Cha ajabu leo nimekaa zangu pale baa nastarehe, hata sijui alipotokea, kaja na kuanza kunichokonoa. Ukweli mimi niliwahi kuwa na uhusiano na Young D kabla yake, yeye akaiba namba kwenye simu yangu wakatongozana mpaka kuwa wapenzi na huenda wameshaachana, sasa sijui kimemuuma nini? Labda alijua angeolewa.”


 
Staa  wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’.
KUNGURU
 “Sitaki kumuongelea huyo mtu, hana maana yoyote nitampa ujiko tu. Yeye alijua rafiki yangu (hakumtaja jina) anatoka na Nay na yeye akajipeleka. Kiko wapi sasa? Mbona kaachwa! Tena ndiyo kwanza kaambulia kusambaziwa picha zake za utupu mitandaoni.

NAY, YOUNG D
Kwa upande wake, Young D alipotafutwa kwa simu na kuambiwa kuhusu wasanii hao aligoma kuwazungumzia. Nay yeye alipoulizwa alianza kwa kucheka, akasema: “Ha! Ha! Mimi sijawahi kuwasikia hao watu na siwajui kabisa labda kuna kitu wanakitafuta kutoka kwangu.”

MANDLA '' MJUKUU WA NYERERE KUFUNGWA AU KULIPA FAINI ...!

 
Mandla Mandela, mjukuu wa kwanza wa aliyekuwa rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.
 
 
 
Mandla akiwa na babu yake Mzee Nelson Mandela.
 
MANDLA MANDELA, mjukuu wa kwanza wa aliyekuwa rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, amehukumiwa kwenda jela au kulipa faini ya kwa kumshambulia na kumtishia kwa bastola mwalimu wa shule moja mwaka 2013.

Mandla, ambaye ni mbunge wa chama tawala cha African National Congress (ANC), alitiwa hatiani kwa kumshambulia mwalimu aitwaye Mlamli Ngudle kutokana na ajali ya barabarani iliotokea huko Mthatha, Jimbo la Cape, Afrika Kusini.

Mwendesha mashitaka alisema mnamno mwezi Machi mwaka huu, Ngudle aliligonga gari lililokuwa limesimama la mmoja wa marafiki wa Mandla, ambapo Mandla alimtishia jamaa huyo kwa bastola, jambo lililomtia hatiani.

Mandla alipigwa faini ya Randi 10,000 (sawa na fedha za Kitanzania kiasi cha shilingi million 1.7), ambapo mpaka sasa ameshalipa Randi 8,000 na kubaki Randi 2,000 (sawa na fedha za kitanzania kiasi cha shilingi 343,000. Endapo ataamua kutokulipa faini iliyobaki, atafungwa jela miaka miwili.

Mandla alijulikana sana mwaka 2013 ambao hakimu mmoja wa mahakama ya Mthatha alimwamuru kurudisha mabaki ya miili ya baba yake na watoto wengine wawili wa Nelson Mandela huko Qunu, ambako ndiyo sehemu yao ya asili.

Mjukuu huyo wa Mandela alikuwa ameihamisha miili hiyo kwenda katika kituo kimoja cha makumbusho bila ya kushauriana na familia yake.

WAGONJWA MUHIMBILI WASOTA .....>>

Hadia Khamis na Johanes Respichius (RCT), Dar es Salaam, Mtanzania gazeti !

 BAADHI ya wagonjwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wamelalamikia hatua ya uongozi wa hospitali hiyo kushindwa kuchukua hatua za dharura za kutoa huduma za CT-Scan, ambayo imeharibika kwa kipindi cha miezi miwili sasa.

 Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti, wagonjwa hao walisema wamekuwa wakiteseka kwa kipindi cha miezi miwili sasa bila kupata huduma hiyo.

 Mmoja wa wagonjwa hao aliyejitambulisha kwa jina la Rashid Omari, alisema ni mwezi wa pili sasa amekuwa akienda na kurudi hospitalini hapo bila ya kupata huduma.
“Kila nikifika bado nakutana na bango la ujumbe unaosomeka mashine ni mbovu mafundi wanafanya matengenezo, nimekuwa nikienda na kurudi huku tatizo likizidi kukuwa, mpaka sasa sijui hatima yangu itakuwaje,” alisema Omari.


 Akizungumza na MTANZANIA Ofisa Uhusiano wa Hospitali hiyo, Aminiel Eligaesha, alikiri kuharibika kwa mashine hiyo na kusisitiza kuwa tayari uongozi umeshaagiza kifaa cha mashine hiyo kutoka nchini Afrika Kusini.
“Tunatarajia kifaa hicho kitafika haraka iwezekanavyo ili kuweza kuwapatia huduma ya kipimo cha CT-Scan wagonjwa wetu wanaokuja kwa ajili ya kufanyiwa kipimo hicho,” alisema Eligaesha.

SAKATA LA MESI LATINGA TFF ...>>>

SAKATA la winga wa timu ya Simba, Ramadhan Singano ‘Messi’, akidai mkataba wake umechezewa na klabu yake hiyo sasa limefika rasmi kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili utata wake kumalizwa.

 Messi amekuwa na mvutano mkubwa na klabu yake akidai mkataba wake wa miaka miwili umechezewa kwa kuongezewa mwaka mmoja zaidi unaoisha Julai mwakani, tofauti na ule alionao yeye unaomalizika mwezi ujao.

                                          MESSI GOAL 

 Katibu Msaidizi wa Chama cha Wanasoka Tanzania (Sputanza), Abeid Kasabalala, aliliambia MTANZANIA kuwa wameshayafanyia kazi malalamiko hayo ya Messi kwa mujibu wa vielelezo alivyoviwasilisha na jana asubuhi wamelipeleka suala hilo TFF kwa ajili ya kufanyiwa uamuzi.
“TFF ndio wenye mpira wao, tumelipeleka suala hilo huko leo asubuhi (jana), wenyewe wamelichukulia kwa uzito mkubwa na wameahidi kulifanyia kazi kwa haraka kwa kulipeleka kwenye kamati husika.
“Suala hilo limefika sehemu nzuri kwani kilichopo TFF watalinganisha mikataba waliyokuwa nayo na ile ya Messi ambayo inadaiwa kuwa na utata, wala hamna kazi kubwa sana tunaamini haki itatendeka,” alisema.


 Uongozi wa Simba kupitia Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Haji Manara, jana ulisema kuwa haujachezea mkataba wa nyota huyo huku ukifika mbali zaidi na kudai wapo kwenye mchakato wa kumwadhibu Messi kutokana na kuichafua klabu hiyo.

 Manara pia alieleza kuwa wanaiomba TFF kutoa tamko kuhusu sakata hilo, kwani wana vielelezo vyote vya mikataba wanayoingia na wachezaji wao akiwemo Messi, huku wakidai wapo tayari suala hilo lichunguzwe na vyombo vya dola.

 Azam FC imeonyesha nia ya kumsajili Messi lakini wamedai kuwa hawataanza taratibu zozote za usajili wake mpaka pale matatizo na klabu yake yatakapomalizika.

 Simba kushusha kifaa Juni 16
Wakati huo huo mshambuiaji mahiri wa timu ya Taifa ya Burundi na klabu ya Vital, ‘O Laudit Mavugo, anatarajia kutua rasmi Simba Juni 16 mwaka huu kumalizana na timu hiyo tayari kwa kujiunga na wenzake kwenye maandalizi ya michuano ya Kagame inayotarajia kuanza Julai 12, Dar es Salaam.


 Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hanspoppe, alisema asilimia kubwa ya mazungumzo yao na mchezaji huyo yamekamilika kinachosubiriwa ni yeye kutua nchini na kutia saini mkataba wake.

“Tumeamua kumwacha kwa muda ili kuweza kukamilisha ratiba ya michuano na timu yake ya Taifa, baada ya hapo atatua nchini kwa ajili ya kukamilisha taratibu zilizobakia,” alisema.

 Alisema kwa sasa wamejipanga kufanya usajili kwa utulivu na hawataki kukurupuka, kwani wanahitaji mabadiliko kuanzia kwenye michuano hiyo ya kiamataifa hadi ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2015/2016.

 Hadi sasa Simba imesajili wachezaji Mohamed Fakhi (JKT Ruvu), Samir Nuhu (Azam), Mohamed Abraham (JKU Zanzibar), Peter Mwalyanzi (Mbeya City) na Mussa Hassan ‘Mgosi’ (Mtibwa).

 Wakati wakijiandaa na michuano hiyo, hatima ya kupatikana kwa kocha mpya, wachezaji watakaoiaga timu hiyo na watakaoenda kwa mkopo kwenye timu nyingine itapatiwa ufumbuzi kwenye kikao cha ndani cha klabu hiyo, kilichofikia tamati jana baada ya kudumu kwa muda mrefu.

 Timu hiyo inatarajia kuanza mazoezi rasmi Jumatatu wiki ijayo Uwanja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kujiandaa na michuano hiyo ya Kagame.

UANDIKISHAJI UNASUA SUA .. MBINU MBADLA ITAFUTWE ... >>

        

Tanzania tuliamua kuandikisha upya wapigakura katika Daftari la Kudumu baada ya kujiridhisha kuwa tulilonalo halifai. Kutokana na ukweli huo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva aliweka bayana kuwa hataendesha uchaguzi wowote kabla ya uandikishaji kumalizika.

Awali, ilitarajiwa kwamba uandikishaji huo ungekamilika kabla ya Aprili 30, siku iliyokuwa imetengwa kwa ajili ya upigaji wa Kura ya Maoni lakini mashine za uandikishaji za BVR zilichelewa na kusababisha mchakato huo kusuasua.

Hivi sasa Tume iko katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu na tayari imeshasema utafanyika Oktoba 25. Kama ilivyo kwa Kura ya Maoni, Uchaguzi Mkuu nao utategemea kukamilika kwa uandikishaji huo.

Makadirio yanasema kuwa wanaotarajiwa kuandikishwa ni watu 24 milioni. Kwa siku 96 kuanzia Februari 24 hadi Mei 31, wameandikishwa watu milioni sita tu na kwa mujibu wa ratiba ya Tume uandikishaji unapaswa kukamilika Julai 18, hivyo ndiyo kusema kuwa zimesalia siku 44 tu kuandikisha watu zaidi ya milioni 18.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu la Taifa (NBS), inakadiriwa kuwa Mkoa wa Dar es Salaam una wapigakura wapatao milioni 2.9. Hao wanatarajiwa kuandikishwa katika Daftari kwa siku 12 tu kuanzia Julai 4 hadi 16. Sababu inayotolewa na NEC ni kuwa eti mashine zote 8,000 za BVR kwa wakati huo zitakuwa Dar es Salaam jambo ambalo halina uhalisia kwani wakati huo ndipo mikoa ya Morogoro, Pwani na Tanga itakuwa inaendelea na uandikishaji.

Takwimu za NBS zinakadiria kuwa Morogoro ina watu wanaostahili kupiga kura wapatao 1.28 milioni wakati Tanga ina wapigakura wapatao 1.12 milioni. Hao wote kwa ujumla wao ni sawa na watu milioni 2.4 idadi ambayo ni ndogo kuliko ya wapigakura wa Mkoa wa Dar es Salaam, lakini huko wamepewa mwezi mzima wa uandikishaji.

Kwa mtiririko huo wa mambo, hatuoni jinsi ambavyo NEC itakamilisha uandikishaji kabla ya Uchaguzi Mkuu. Hofu hiyo wanayo Watanzania wengi, lakini kama kawaida Tume imekuwa bingwa wa kuweka nta masikioni.

Tunaitaka iongeze kasi ya uandikishaji ili kuwapa matumaini Watanzania hasa kwa sababu uzoefu unatuonyesha kuwa katika maeneo ambayo tayari uandikishaji umekamilika ilibidi ziongezwe siku kwa sababu wapigakura waliojitokeza ni zaidi ya makadirio.

Hivyo, kwa makadirio yasiyo rasmi yawezekana wapigakura wakawa zaidi ya milioni 27. Kama hivyo ndivyo, NEC inabidi ijipange upya na iweke nguvu zaidi kukabiliana na changamoto hiyo, kinyume chake kuandikisha watu zaidi ya milioni 20 kwa siku 44 zilizosalia ni ndoto. Hata kama ikibadili ratiba na kusema itaandikisha mpaka Oktoba 24 bado siku hizo hazitoshi kutokana na mwenendo wenyewe wa uandikishaji unavyoendelea.

Hadi sasa bado malalamiko ya misururu mirefu katika vituo vya uandikishaji yanaendelea sambamba na waandikishaji kuchukua zaidi ya nusu saa kuandikisha mtu mmoja, hali hiyo inadhihirisha kuwa tumefanya makosa kufanya jambo kubwa kama hili la uandikishaji upya wapigakura mwaka wa uchaguzi.

Mambo yamekuwa mengi, tumejizonga na kuzongeka na sasa joto la wasiwasi linazidi kupanda. Ndiyo maana tunasema tunapaswa kutafuta mpango B mapema kabla hatujaenda mrama.

UZI MPYA WA TAIFA STARS ..... >>>

 

Hamasa na mapenzi makubwa waliyokuwa nayo Watanzania kwa timu yao ya Taifa, Taifa Stars yamepotea siku za karibuni kutokana na sababu mbalimbali, zikiwamo matokeo mabaya ya timu hiyo.
Hilo, limemfanya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Said Mtanda afikirie kivingine na kutoa ushauri.
Jana, Mtanda aliyekuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya uzinduzi wa jezi mpya za Stars alitaka mashabiki na wadau wengine wa soka kurejesha mapenzi yao kwa Taifa Stars.
Uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam ulikwenda sanjari na utoaji vyeti kwa makundi mbalimbali ya watu, waliotoa mchango wao kwenye maendeleo ya mchezo wa soka nchini.
Katika uzinduzi huo, kulizunduliwa jezi aina tatu, ambazo ni jezi za ugenini, jezi za nyumbani na jezi zitakazokuwa zikitumika kwa ajili ya mazoezi.
Mtanda, ambaye ni Mbunge wa Mchinga mkoani Lindi alisema uzinduzi wa jezi hizo uwe chachu ya kurudisha hamasa na mvuto wa timu ya Taifa kwa Watanzania.
Alisema kuwa anaamini mabadiliko hayo ya jezi yatakwenda sanjari na hatua madhubuti za kuziimarisha timu mbalimbali za Taifa zifanye vizuri katika mashindano mbalimbali zitakayoshiriki.
“Kuna watu wanahoji hivi tunahitaji jezi mpya au timu yetu ya Taifa kufanya vizuri? Mimi naona tunahitaji vyote viwili. Tubadilishe namna ya kuendeleza timu yetu ya Taifa pia tubadilishe jezi zinazotumiwa Taifa Star,” alisema Mtanda.
Jezi hizo zitaanza kutumiwa na Stars kwenye maandalizi yao ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) na Michezo ya wachezaji wa ndani (Chan), zitakuwa ni nyeupe kwa mechi za ugenini, wakati kwa mechi za nyumbani zitakuwa za rangi ya bluu.
Akizungumza baada ya uzinduzi huo, kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij alisema kuwa kikosi chake kiko tayari kwa ajili ya kupeperusha vyema bendera ya nchi katika mashindano yanayoikabili.
Nooij alisema kuwa kila mmoja kikosini anatambua deni ambalo timu hiyo inalo kutoka kwa mamilioni ya Watanzania, hivyo watapambana kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mechi hizo dhidi ya Misri na Uganda.

“Tunaendelea na maandalizi yetu na molali ya wachezaji iko juu. Wachezaji wanaendelea kuimarika siku hadi siku na kila mmoja wetu anajituma kwa kadri ya uwezo na majukumu yake ili tuwape furaha Watanzania,” alisema.

PINDA AIPA WAKATI MGUMU CCM BUNDA .....



Waziri Mkuu Mizengo Pinda atakipa wakati mgumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Bunda, baada ya baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo kutishia kuwa hawatakipigia kura kutokana na kiongozi huyo kutoa ahadi hewa ya upatikanaji wa maji safi na salama.
                              
Wakazi hao wameapa kuwa labda ahadi hiyo iliyotolewa na Waziri Pinda Machi mwaka jana, itekelezwe kabla ya Uchaguzi Mkuu, kinyume cha hivyo hawataipigia kura CCM ili kuonyesha kuwa hawaridhiki na namna wanavyodanganywa.

Wakazi hao walitoa tishio hilo juzi katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM akiwamo, Katibu wa CCM mkoa wa Mara Adam Ngalawa na Naibu Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mfaume Kizigo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mkutano huo, walisema, wameazimia kutoipigia kura CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba kwa kuwa viongozi wa CCM na Serikali yake wanatoa ahadi za uongo na zisizotekelezeka.

Michael Kweka alitaja ahadi iliyotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda Machi mwaka jana kwamba tatizo la maji lingekoma Juni, kuwa ni moja ya ahadi hewa za viongozi wa Serikali ya CCM zinazowachefua wananchi.

“Hatutawapigia kura za urais, ubunge wala udiwani wagombea wote watakaoletwa na CCM mwaka huu kwa kuwa wanakuwa wakitudanganya kwa ahadi hewa,” alisema Kweka.

Kweka alisema akiwa ziarani wilayani Bunda Machi mwaka huu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitoa ahadi kwamba tatizo la maji lingekwisha ifikapo Juni mwaka huu, lakini hadi sasa hakuna dalili zozote za kumaliza kero hiyo.

Alisema hali hiyo inawafanya wakazi wa mji huo ambao wamekuwa wakidamka nyakati za usiku kutafuta huduma ya maji safi na salama kuichukia Serikali ya CCM, wakiamini kuwa haiwajali. “Mimi kero yangu ni maji. Hiki kimekuwa kilio chetu kwa muda mrefu.

Lakini kinachotuumiza ni ahadi hewa za viongozi wa Serikali ya chama chetu cha Mapinduzi kuhusu mradi unaotekelezwa hapa. Mnaonaje tukiwanyima kura sababu mmezidi ubabaishaji,” alisema mkazi mwingine wa eneo hilo akiwahoji viongozi wa CCM waliokuwapo meza kuu.

Nyerere Lucas aliilalamikia Serikali ya CCM kwa kile alichoeleza kuwa imeshindwa kutimiza ahadi zake za kuboresha miundombinu ya barabara wilayani humo kama ilivyoahidi katika Uchaguzi Mkuu uliopita na kuwafanya wakazi wa maeneo hayo kusafiri kwa tabu kutafuta maji mbali na maeneo yao. Kero nyingine walizolalamikia wakazi wa wilaya hiyo ni mikopo kwa vijana na akinamama.

Walisema mikopo kwa makundi hayo imekuwa ikitolewa kwa watu maaalum hasa vikundi vinavyomilikiwa na watumishi wa serikali, jambo ambalo limeonekana kwamba kuna nia ya dhati ya kuwasahau wananchi.

Hata hivyo, Katibu wa CCM mkoa wa Mara, Adam Ngalawa katika majibu yake ameshindwa kueleza lini mradi huo wa maji utakamilika badala yake akasema umepangwa kutekelezwa katika bajeti ya mwaka 20015/16.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Mfaume Kizigo aliwataka viongozi wa chama hicho ngazi zote kutokaa ofisini badala yake waende kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuzitafutia majawabu.

viongozi hao wa CCM walikuwa katika ziara ya kukijenga chama katika wilaya ya Bunda mkoani Mara.