Wednesday, 11 February 2015

ETI BODA BODA NI SEREKALI ? AU AJIRA RAHISI KWA WATANZANIA WALIO WENGI ZAIDI ?



 GAZETI MWANANCHI ...Kama kuna eneo ambalo tunadhani Serikali imeonyesha udhaifu mkubwa ni udhibiti wa usafiri wa pikipiki, maarufu kama Bodaboda. Waendesha Bodaboda hapa nchini sasa wanaweza kufananishwa na ‘serikali’ inayojitegemea yenye ‘jeshi’ la ulinzi na usalama.

Tofauti iliyopo ni kwamba ‘serikali’ ya Bodaboda inaongozwa na kanuni na sheria za msituni za kulipiza visasi. Kama habari tulizochapisha katika matoleo ya tovuti hii juzi na leo zinavyoonyesha, udhaifu huo wa Serikali umetoa mwanya kwa waendesha Bodaboda kuunda utawala wao katika nyanja za ulinzi na usalama, biashara na hata masuala ya kijamii kama magonjwa na vifo.

Utawala wao uko nje kabisa ya mfumo rasmi wa utawala wa sheria tuliouzoea katika nchi yoyote inayoendeshwa kwa katiba ya nchi na sheria za kimataifa. ‘Serikali’ ya waendesha Bodaboda ndio mwendesha mashtaka, mahakama na hata magereza. Kwa mfano, uchunguzi wetu umebaini kuwa, inapotokea ajali kati ya dereva wa gari na mwendesha Bodaboda,  kundi la waendesha Bodaboda litatoka huko litokako na kuanza kutoa kipigo kwa dereva wa gari na wakati mwingine kulichoma moto gari hilo au kuliharibu.
Katika uchunguzi huo, imebainika kwamba umoja huo  umetokana na waendesha Bodaboda kujenga dhana kwamba jamii inawachukia na madereva wa magari wanawagonga makusudi kwa nia ya kuwakomoa. Waendesha Bodaboda wamekuwa wakipoteza maisha au kupata majeraha ya kudumu katika ajali za barabarani. Taarifa za Jeshi la Polisi nchini zimethibitisha kuwapo watu wengi wanaopoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya katika ajali hizo. Kwa mfano, takwimu za ajali hizo mkoani Dar es Salaam zimeonyesha kuwa, wastani wa watu watatu wanakufa kila siku kutokana na ajali zinazohusisha Bodaboda.
Ndio maana waendesha Bodaboda wanaonekana wakiandamana pale inapotokea mwenzao amegongwa na gari, kuuawa baada ya kuibiwa pikipiki au kufanyiwa jambo lolote linaloonekana kwao kama uonevu. Maandamano hayo pia yanaonekana wakati wakienda kumzika mwenzao aliyekufa ajalini au kwa ugonjwa. Uchunguzi wetu umeonyesha kwamba mazingira hayo yamewalazimisha kuweka ‘polisi’ wa kituo katika kila kituo cha Bodaboda na viongozi wengine wanaoitwa wenyeviti na makatibu. Uchunguzi umegundua kwamba akitokea dereva mwenzao akaibiwa pikipiki au akagongwa na gari, ‘polisi’ atawakusanya wenzake na hatimaye kuanzisha mashambulizi kwa mtuhumiwa.

Lakini kama habari tuliyochapisha gazetini leo inavyosema, Bodaboda pia zimetumika katika matukio mengi ya uhalifu. Baadhi ya waathirika wa uhalifu huo wametoa ushuhuda na kusema kuna haja ya kudhibiti usafiri huo, vinginevyo utaleta maafa.  Kutokuwapo udhibiti kumezalisha madereva wa Bodaboda ambao wanaweza kulinganishwa na watu wasiojitambua, mithili ya vichaa waliobeba mapanga na majambia kisha kumwagwa katikati ya umati mkubwa wa watu. Wengi hawana elimu ya sheria za usalama barabarani, hawana leseni wala bima na wanashindia viroba na misokoto ya bangi.

Lazima tukubali kwamba usafiri wa Bodaboda utaendelea kuwapo, kwani pia umerahisisha usafiri mijini na vijijini. Kuupiga marufuku kutaumiza wananchi na kukaribisha maafa ya vijana hao kurudi mitaani na kunyonga watu. Serikali inachopaswa kufanya ni kuanzisha kitengo maalumu ndani ya Kikosi cha Usalama Barabarani kuratibu usafiri huo. Waendesha Bodaboda wasajiliwe, wapewe mafunzo na wavae sare maalumu, huku Bodaboda na abiria wao wakilazimika kisheria kuvaa kofia ngumu. Ni jukumu la Serikali kuhakikisha waendesha Bodaboda pia wanaheshimu sheria za nchi.

No comments:

Post a Comment