Jeshi la Polisi mkoani hapa limefunga vituo vitatu katika eneo la Nkuhungu baada ya kubaini uwepo wa watoto na vijana 115 kutoka mikoa 13, ikiwa ni pamoja na visiwani Zanzibar, waliokuwa wakilelewa kwenye mazingira hatarishi.
Hata hivyo, kubainika kwa watoto hao ni tofauti na
matukio ya mkoani Kilimanjaro ambako Jeshi la Polisi lilibaini zaidi ya
watoto 200 waliokuwa wamefungiwa kwa miaka takriban mitatu wakipewa
mafunzo ya kisiri na hivyo kuibua hisia za ugaidi.
Katika tukio la Dodoma, polisi imesema inaendelea na uchunguzi kujua walichokuwa wakifundishwa vijana hao.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake
jana, kamanda wa polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema watoto
hao wanatoka katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Mtwara,
Kagera, Tanga, Tabora, Singida, Pwani, Lindi, Geita, Mwanza na Manyara.
Alisema baada ya kupokea taarifa ya uwepo wa
watoto hao, walifika katika vituo hivyo saa 6:30 usiku jana na kukuta
watoto hao wenye umri wa chini ya miaka 25.
“Polisi iligundua vituo vitatu katika eneo la
Nkuhungu, Dodoma Mjini baada ya kupokea taarifa kwamba kuna nyumba
ambazo zinaonekana kuingia watoto wengi na inawezekana siyo mazingira
salama ya kuishi binadamu hasa watoto na wanachofundishwa huenda ni
kinyume cha maadili,” alisema.
Kamanda Misime alisema katika vituo hivyo
walipatikana jumla ya watoto 63 wenye umri wa chini ya miaka 18, wakati
walio na vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 na 25 walikuwa ni 52.
Alifafanua kuwa kati ya watoto hao waliotoka Wilaya ya Kondoa mkoani
hapa ni 50 wakati waliotoka wilaya za Dodoma Mjini, Chamwino na Mpwapwa
ni watoto 26.
“Uchunguzi unaendelea na yeyote atakayeguswa na
ushahidi kuwa amekiuka sheria atafikishwa mahakamani, wakiwemo wazazi
walioruhusu watoto kuwa katika uangalizi ambao siyo wa kutosha kama
sheria ya watoto ya mwaka 2009 inavyoelekeza,” alisema.
Pia alisema jeshi hilo linachunguza watoto hao
walikuwa wakifundishwa kitu gani na kama walikuwa wakihudhuria shule
kulingana na umri wao na sheria za nchi zinavyoelekezwa.
Ingawa hakulihusisha tukio hilo na mafunzo ya
ugaidi, Kamanda Misime aliwataka viongozi na watu wataka maeneo kama
hayo katika himaya zao na vituo visivyosajiliwa ambavyo ni hatarishi kwa
watoto, watoe taarifa mapema.
Pia alitoa wito kwa familia, viongozi wa serikali
za mitaa, dini na taasisi nyingine kutoruhusu watoto wao kupelekwa na
kuelelewa katika vituo hatarishi.
Aidha, aliwataka wazazi wanaofahamu watoto hao wajitokeze ili kupewa maelekezo kabla ya kutafutwa na mkono wa dola.
No comments:
Post a Comment