ZAIDI ya kaya 700 katika Kata ya Arusha Chini TPC, Wilaya ya Moshi,
Mkoa wa Kilimanjaro, hazina makazi baada ya nyumba zao kuharibiwa na
mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha juzi.
Pamoja na madhara hayo kwa wananchi, pia mafuriko hayo yameharibu
miundombinu ya Kiwanda cha Sukari cha TPC, taasisi mbalimbali pamoja na
mashamba ya mazao ya chakula.
Taarifa hiyo ilitolewa jana na Ofisa Mtendaji na Utawala wa Kiwanda
cha TPC, Jaffari Ally, alipokuwa akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya
Moshi, Novatus Makunga, aliyetembelea maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko
hayo.
“Kwa eneo langu la kiwanda, wafanyakazi wangu zaidi ya 600 hawana makazi
na ukija kwenye miundmbonu ya kiwanda, imeharibiwa kwa kiwango
kikubwa kwani barabara, reli pamoja na mashamba yameharibiwa pia.
“Kwa ujumla, mafuriko haya yamechangiwa na mvua kubwa iliyonyesha mkoani
Arusha na hapa Kilimanjaro kwa ukanda wa juu kwani eneo hilo lina
makutano ya Mito ya Weruweru, Karanga na Kikavu,” alisema.
Naye, Makunga alisema wananchi walioathiriwa na mafuriko hayo wako
katika Vijiji vya Kata ya Arusha Chini TPC ambavyo ni River Side, Kijiji
cha
Kati, Langasani Magharibi na Mashariki.
“Kwa asilimia kubwa, maji yaliyosababisha mafuriko haya yametokana na
mvua iliyonyesha Mkoa wa Arusha na mito mingi ilishindwa kuyahimili na
hivyo kingo kuharibika na maji kuvamia makazi ya watu.
“Hata hiyo, hasara iliyotokana na mafuriko haya kwa upande wa kiwanda
cha sukari pamoja na wananchi, bado haijajulikana kwa sababu tathmini
bado inaendelea,” alisema Makunga.
Kutokana na uharibifu uliotokea, alisema wananchi walioharibiwa makazi
yao wamehifadhiwa katika sehemu ya kiwanda cha TPC ambayo haikuathiriwa.
Kwa upande wake, mdau wa maendeleo katika Jimbo la Moshi Vijijini, Ansi
Mmasi, alisema kuna haja ya Serikali kuangalia namna ya kukabiliana na
mafuriko hayo kabla hayajaleta madhara zaidi.
No comments:
Post a Comment