Tuesday, 10 February 2015

TAJIRI GATES AMUA KUPAMBANA NA MARADHI ...>>

Bill Gates anuia kuyapiga vita maradhi 

Gazeti la "Die Zeit " linatuarifu juu ya dhamira ya tajiri mkubwa duniani, Bill Gates ya kuwasaidia masikini.Gazeti hilo linauliza jee tajiri huyo ataweza kweli kuwaepusha masikini na maradhi ya hatari?
Gazeti hilo linakumbusha kwamba mkutano juu ya kile kinachoitwa mfungamano wa chanjo za kukinga maradhi, Gavi ulifanyika hivi karibuni mjini Berlin. Mwenyeji wa mkutano alikuwa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Gazeti la "Die Zeit" linasema viongozi kutoka nchi mbalimbali hasa za Afrika pia walikuwapo kwenye mkutano huo.Lakini mgeni muhimu kabisa hakuwa kiongozi wa nchi yoyote, na wala halikuwa Shirika la Afya Duniani, WHO, bali ni Wakfu wa Bill na Melinda Gates.

Gazeti la "Die Zeit" limearifu kuwa kuanzia mwaka ujao hadi mwaka 2020 Wakfu wa Bill na Melinda Gates utatoa dola Bilioni saba na nusu kwa ajili ya kuutekeleza mradi wa chanjo, maarufu kama Gavi katika nchi za Afrika. 

Lengo la Wakfu wa Bill na Melinda, linasema gazeti la "Die Zeit" ni kupambana na umasikini,maradhi na vifo vya mapema.Lakini gazeti hilo limeuliza jee tajiri mmoja peke yake ataweza kupambana na maadui hao wakubwa wa binadamu?

Mwandishi:Mtullya Abdu. Deutsche Zeitungen.
Mhariri: Josephat Charo

No comments:

Post a Comment