MCHAKATO wa kupata Katiba Mpya ya nchi unadaiwa kugubikwa na wingu la
ufisadi hali iliyosababisha Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma
(PPRA) kuhoji tenda ya uchapwaji wa nakala milioni mbili za Katiba
Inayopendekezwa kwa gharama ya Sh bilioni 6.
Hatua hiyo inakuja huku Watanzania wakiwa wanasubiri kupiga kura ya
maoni inayotarajiwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu, ambapo inaelezwa
taratibu za manunuzi zilikiukwa kwa baadhi ya kampuni zilizopewa kazi
hiyo kuwa na walakini.
Kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011, taasisi zote za
umma zinatakiwa zitangaze zabuni kabla ya kutoa zabuni husika.
Kutokana na sheria hiyo, inaelekeza taarifa za zabuni husika hutangazwa
kupitia jarida na tovuti ya PPRA jambo ambalo linadaiwa halikufanywa na
Wizara ya Katiba na Sheria.
Chanzo cha kuaminika kiliiambia MTANZANIA kuwa kazi ya uchapaji wa
nakala hizo za Katiba Inayopendekezwa ilianza kufanyika tangu Desemba
mwaka jana.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kila nakala ya Katiba Inayopendezwa inachapishwa kwa gharama ya Sh 3,000.
“Kwenye hizo kampuni zilizopewa hiyo kazi, nyingine hata uwepo wake una
walakini, hii haikuwa kazi ya dharura kiasi hicho, lakini pia kutoa
zabuni ya Sh bilioni 6 za umma kwa kujuana tu bila kufuata taratibu ni
jambo la kushangaza,” kilipasha chanzo chetu.
Pamoja na hali hiyo, lakini inaelezwa Wizara ya Katiba na Sheria
imeshindwa kutoa kazi hiyo kwa Mpigachapa Mkuu wa Serikali kama
ilivyoahidiwa na Serikali mapema mwaka jana.
MTANZANIA ilimtafuta Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa PPRA, Mcharo Mrutu,
ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, ambaye alisema PPRA tayari
imeiandikia barua Wizara ya Katiba na Sheria kupata taarifa za kina juu
ya taratibu za utangazaji wa zabuni hiyo.
“Tumewaandikia barua Wizara ya Katiba na Sheria ambao ndio waliotoa hiyo
kazi, baada ya maelezo yao ya kina ndiyo tunaweza kuwa katika nafasi
nzuri ya kulizungumzia suala hilo,” alisema Mrutu.
Akizungumzia suala hilo, Msemaji wa Wizara ya Katiba na Sheria, Omega
Ngole, alisema katika kutoa zabuni hiyo sheria na taratibu zote
zilifuatwa, na wahusika wote muhimu walijulishwa ikiwamo PPRA na
Mpigachapa Mkuu wa Serikali.
“Ninavyofahamu mimi, sheria ya manunuzi na kanuni zake na miongozo ya
Serikali kuhusu manunuzi ilifuatwa kikamilifu ikiwamo kumshirikisha
Mpigachapa Mkuu wa Serikali ambaye ndiye mchapaji mkuu wa nyaraka za
Serikali,” alisema.
Alipotafutwa Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo, ambaye
ofisi yake inadaiwa kutafuta wachapishaji hao, alisema wahusika wakuu
katika suala hilo ni Wizara ya Katiba na Sheria na PPRA, kwamba ndio
wanaoweza kujibu suala hilo.
“Kama una shaka na suala hili, hatua uliyochukua ni sahihi, watu wa
sheria ndio watu sahihi kabisa kwa sababu ndio wanaoshughulikia suala
hili na wanaweza kukwambia kama taratibu zilifuatwa ama la,” alisema
Chibogoyo.
Alipoambiwa Wizara ya Katiba na Sheria imerusha mpira kwa ofisi yake,
Chibogoyo alihoji: “Unaposema Katiba na Sheria unamaanisha nani, kwa
maana ya Wizara ya Katiba na Sheria?
“Kama PPRA wamesema wanataka maelezo zaidi, kuna maelezo yatapelekwa huko na watakuwa na cha kusema,” alisema.
Mtanzania: Kwahiyo ofisi yako haina chochote cha kusema?
Chibogoyo: Mimi ninachoweza kukwambia tu ni kwamba umefuata taratibu
sahihi kwa watu uliowauliza hili suala, kama kutakuwa na jingine kwa
ufafanuzi watatoa.
Mtanzania: Lengo la kutaka kauli yako ni kwa sababu wewe ndiyo
mpigachapa mkuu, na hili jukumu ni lako na hizo kampuni tatu umetafuta
wewe, ndiyo maana tunataka kauli yako.
Chibogoyo: Haya mambo kama una taarifa ambazo ni muhimu kwa jamii njoo
ofisini kwangu, ujieleze pale na mimi naweza kuchangia kitu,
nikikukaribishe tu ofisini kwangu kesho.
Chanzo chetu cha habari kilisema baada ya kutolewa kwa kazi hiyo ya
kuchapa Katiba Inayopendekezwa kwa kampuni binafsi, nyaraka zinazoenda
serikalini husomeka kuwa Serikali imenunua karatasi kwa kampuni hizo,
badala ya kusomeka kuwa kazi husika imechapwa na kampuni hizo.
Februari 7, mwaka huu, akiahirisha Bunge mjini Dodoma, Waziri Mkuu
Mizengo Pinda, alisema Serikali itachapisha nakala milioni mbili za
Katiba Inayopendekezwa ambazo zitasambazwa kwa watu mbalimbali nchi
nzima.
Alisema hadi sasa tayari nakala 654,024 zimechapishwa na kugawanywa kwenye mikoa 11 nchini.
No comments:
Post a Comment