Monday, 11 May 2015

Hon . E. LOWASSA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU NA HISTORIA YAKE HII HAPA ...>>

Historia yake
Edward Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 katika Kijiji cha Ngarash, Monduli na ndiye mtoto mkubwa wa kiume kwa Mzee Ngoyai Lowassa (atafikisha miaka 62 Agosti mwaka huu). Alianza kusoma katika Shule ya Msingi Monduli kati ya mwaka 1961–1967.
Kisha akaendelea kwenye Shule ya Sekondari Arusha kwa kidato cha kwanza mpaka cha nne kati ya mwaka 1968 - 1971, kabla ya kumalizia kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Milambo mkoani Tabora mwaka 1972–1973.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1974–1977 na kuhitimu Shahada ya Sanaa katika Elimu (B.A Education) na baadaye Chuo Kikuu cha Bath Uingereza kwa Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Maendeleo (mwaka 1983–1984).
Baada ya kumaliza chuo kikuu, Lowassa alifanya kazi ndani ya CCM akiwa ofisa wa ngazi ya juu kuanzia wilaya, mkoa na baadaye makao makuu kati ya mwaka 1977–1989.
Aliajiriwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC), mwaka 1989–1990.
Lowassa amemuoa Regina na wana watoto watano, wasichana wawili na wavulana watatu. Watoto hao ni Fredrick, Pamella, Adda, Robert na Richard.

Mbio za ubunge
Lowassa alichaguliwa kuwa Mbunge wa Monduli mwaka 1990 na 1993 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (Haki na Mambo ya Bunge), kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ardhi na Makazi akiwa Waziri mwaka 1993–1995.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi (mwaka 1995), Lowassa alishinda ubunge kwa asilimia 87.3. Alikaa bila uteuzi wowote kwa miaka miwili. Mwaka 1997–2000, Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Kuondoa Umasikini).
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 aligombea tena ubunge wa Monduli na kushinda kwa mara ya tatu. Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Maji na Mfugo hadi mwaka 2005.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2005, aligombea ubunge na kushinda kwa asilimia 95.6. Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Bunge likamthibitisha kwa kura 312.

Uwaziri mkuu wa Lowassa ulikoma Februari 2008, alipojiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond. Kamati Maalumu ya Bunge ya watu watano iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe ilisisitiza kuwa wizara ya Nishati na Madini na Ofisi ya Waziri Mkuu ndizo zinazopaswa kubeba lawama ya uingiaji wa mkataba mbovu na Richmond, kampuni ambayo uchunguzi ulionyesha kuwa ni ya mfukoni mwa watu huku Serikali ikilazimika kulipa mabilioni ya fedha katika mkataba ambao una upungufu makubwa.
Wakati Lowassa analitaarifu Bunge kuwa amemuandikia Rais barua ya kujiuzulu, alisisitiza kuwa “…anafanya hivyo ili kulinda taswira ya chama chake na Serikali na kuwa shida ya wabaya wake ni u-waziri mkuu na siyo kingine…”

Baada ya kujiuzulu, Lowassa aligombea ubunge kwa mara nyingine Monduli (mwaka 2010) na kupata asilimia 90.93 ya kura zote na hadi sasa ndiye mbunge wa jimbo hili japokuwa amekwishaaga kwamba hatagombea tena kiti hicho.

Mbio za urais
Lowassa ni miongoni mwa wana CCM 17 waliochukua fomu kuwania urais mwaka 1995 lakini aliyepitishwa ni Mkapa.
Mwaka 2005, hakugombea urais ila alikuwa na mipango ya muda mrefu ya kumsaidia rafiki yake, Kikwete na inadaiwa kuwa makubaliano ya Kikwete na Lowassa yalikuwa kwamba mwenzake akishaongoza nchi kwa miaka 10 (yaani 2005 – 2015) atamtengenezea njia 2015 – 2025.
Kabla mipango hiyo haijatimia ndipo Lowassa akapata kile ambacho Kikwete anakiita “ajali ya kisiasa”. Lakini hata baada ya ajali ya kisiasa kutokea, nimeambiwa walikuwa na makubaliano mengine kuwa “Kikwete angesaidia kumsafisha rafiki yake” ili mwaka huu 2015 ufikapo aweze kumuachia Ikulu ya Magogoni.
Tangu Lowassa aachie uwaziri mkuu na tangu agundue kuwa Kikwete ‘amemkalia” kimya, alianza juhudi zake mwenyewe za kujitengenezea njia ya kuelekea Ikulu na amefanya mambo mengi yanayoashiria kuwa amedhamiria kuingia Magogoni.
Kama kuna mtu nchi hii ametoa michango mingi ya rasilimali fedha katika kuchangia misikiti, makanisa, vijana, vikundi, harambee na vinginevyo, hakuna kama Lowassa. Michango hiyo, wachambuzi wengi wanaihusisha na mbio zake za urais.

Nguvu yake
Nguvu ya kwanza ya Lowassa ni umaarufu, yeye ni maarufu kuliko wagombea wote wa CCM, ndani na nje ya chama hicho. Yeye ndiye anatajwa kuliko wenzake wote na hili halina shaka.
Nguvu ya pili ya Lowassa iko kwenye uwezo wa kirasilimali (watu na fedha). Lowassa na mtandao wake wana rasilimali za kutosha kuendesha harakati hizi. Kwa siasa za CCM ya miaka hii iliyowatupa mkono wakulima na wafanyakazi, rasilimali (fedha na watu) ni kila kitu. Jambo hili linampa nguvu zaidi dhidi ya wagombea wenzake ambao nao wanahaha huku na kule kuzisaka.

Jambo la tatu linalompa Lowassa nguvu ni kuwahi kuwa Waziri Mkuu na kuijua kwa undani mifumo ya uendeshaji wa nchi na hata kuisimamia. Ushawishi wake kwa mifumo hiyo umeendelea hadi sasa na nimeambiwa kuwa kuna taasisi muhimu za kidola zimegawanyika kwa sababu ya kumuunga mkono, watendaji serikalini nao wamegawanyika kwa ajili yake na kila mmoja ana hofu kuwa asipofanya “booking” kwenye kambi ya Lowassa, anaweza kukosa vyeo bwerere kwenye Serikali ijayo.
Alipokuwa Waziri Mkuu alionyesha misimamo ya kiuongozi na kuthubutu kwingi kunakotakiwa kufanywa na mkuu wa nchi, lakini misimamo yake na uthabiti wake unahusishwa pia na kujikuta mara nyingi akifanya uamuzi wenye makosa mengi au wenye kuzua maswali mengi ya kisheria.
Lakini jambo la nne ni kuzijua njia zilizompa madaraka Kikwete mwaka 2005. Kati ya wagombea wote wa CCM kwa sasa, huenda ni Lowassa peke yake ndiye anayezijua vizuri njia alizotumia Kikwete kujenga mtandao mkubwa wa ushindi mwaka 2005, makanisani, misikitini, vyuoni na kwingineko, hadi nyumba za ibada zikaimba “Kikwete ni chaguo la Mungu”. Kwa hiyo anajua njia ipi apite kuwashinda wagombea wengine.





No comments:

Post a Comment