Gwaride la kuadhimisha sherehe hizo lilifanyika
Jumamosi mjini Moscow na viongozi 20 duniani walihudhuria, akiwamo Ban
Ki-moon, Rais Xi Jinping wa China na Rais Raul Castro wa Cuba.
Maadhimisho hayo yamepewa jina la ‘siku ya kumbukumbu na maridhiano’, huku mvutano kati ya Urusi na nchi za Magharibi ukiendelea kuhusu mzozo wa Ukraine.
Kutokana na kuwapo kwa mzozo huo, nchi za
Magharibi zimesusia sherehe hizo mjini Moscow licha ya Urusi kutoa
mchango mkubwa wa kumaliza vita hivyo.
Katika mji wa Berlin, Bunge la Ujerumani liliiadhimisha siku hiyo baada ya jeshi lake kujisalimisha bila masharti.
“Mei 8, mwaka 1945 ilikuwa siku ya ukombozi barani
Ulaya. Tunaomboleza leo baada ya mamilioni ya watu kupoteza maisha
kwenye vita hivyo wakiwamo Wayahudi wa Ulaya,” alisema Spika wa Bunge la
Ujerumani, Norbert Lammert.
Spika huyo aliwalaumu raia wa Ujerumani kwa kumuunga mkono Adolf Hitler katika vita hiyo.
Spika Lammert alisema: “Siku ya leo si siku ya
ukombozi wa Ujerumani tu bali maadhimisho haya yanakumbusha majaribio
machache yaliyofanywa na baadhi ya Wajerumani ya kutaka kumuua Hitler na
waliofanya majaribio hayo wanapaswa kupongezwa na kutukuzwa.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Kansela Angela Merkel na maofisa
kadhaa wa ngazi za juu wa Ujerumani.
Wakati huohuo, sherehe hizo pia, zilifanyika
Poland jana katika mji wa Gdansk na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon, Rais wa Umoja wa Ulaya (EU), Donald Tusk
na rais wa Ukraine. Pia, nchi nyingine za Ulaya ya Mashariki
zilihudhuria maadhimisho hayo. Mji huo ni wa kwanza kwa raia wake
kuathirika na vita hivyo chini ya majeshi ya Kinazi, mwaka 1939.
Vita vya Pili ya Dunia ilianza baada ya wanajeshi
wa Ujerumani kuingia Poland Septemba 1939 na kumalizika Mei 8, 1945
baada ya Mkuu wa majeshi wa Ujerumani, Wilhelm Keitel, kusaini waraka wa
kujisalimisha usiku wa manane kwenye makao makuu ya Jeshi la Kisovieti
mjini Berlin.
Licha ya kuwapo kwa makubaliano ya kumaliza vita barani Ulaya, mgogoro huo uliendelea barani Asia hadi Agosti 1945.
No comments:
Post a Comment