KAMA wewe ni mpenzi wa Chelsea ukisoma hapa utaumia moyo, lakini
kwa mashabiki wa klabu nyingine za soka la England watachekelea.
Kicheko cha mashabiki wa Chelsea ndio kwanza kimeshamiri baada ya kutwaa
ubingwa wa Ligi Kuu England, lakini kabla hawajakaa sawa ghafla kocha
Jose Mourinho anaibuka na kusema; Eti nikae hapa Stamford Bridge kwa
miaka mingi kama Alex Ferguson (Man United) na Arsene Wenger (Arsenal)!
Msahau hilo.”
Kocha huyo amekiri kwamba lengo lake ni kukiandaa
kikosi na kuwa katika kiwango cha juu lakini haoni kama anaweza kukaa
kwa miaka 20 kwenye klabu hiyo. Mourinho anasema siku hizi mambo
yamebadilika. Na suala la kukaa kwenye timu kwa miaka mingi ni jambo
ambalo limepitwa na wakati.
Kocha wa zamani wa Manchester United Alex Ferguson
aliachana na timu hiyo 2013 baada ya kuinoa kwa miaka 27 na Wenger
ametimiza miaka 19 tangu aanze kuinoa Arsenal.

“Tusidanganyane jamani, jambo hilo haliwezekani. Soka la sasa limebadilika sana,” alisema kocha huyo alipoulizwa iwapo ana mpango wa kukaa kwenye kikosi hicho kwa miaka mingi ijayo.
Alipoulizwa iwapo Wenger atakuwa kocha wa mwisho
kuishi kwenye klabu moja kwa miaka mingi alijibu, “Nadhani ndio hivyo,
maisha yamebadilika.”
Katika hatua nyingine kocha huyo mwenye umri wa
miaka 52 anatarajia kusaini mkataba wa miaka minne kwenye klabu yake
baada ya kumalizika kwa ligi. Kocha huyo amesema kuwa kitu kinachoweza
kumfanya akae kwa muda mrefu kwenye klabu hiyo ni mpango wake wa
kuhakikisha klabu inakuwa na kizazi kipya kinachotikisa dunia.
Hata hivyo uhusiano wa kocha Jose Mourinho na
mmiliki wa kilabu Roman Abramovich kwa sasa ni mkubwa kuliko siku za
nyuma. Abramovich anafurahia uwezo wa kocha huyo wa kutengeneza timu
kubwa na hilo lilithibitika katika awamu ya kwanza ambayo kocha huyo
aliongoza Chelsea. Kocha huyo alitimuliwa mwaka 2007 na wakati
anatimuliwa aliacha kikosi imara alichokitengeneza mwenyewe. Kikosi
hicho kilisonga mbele na kupata ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi
ya Europa na vikombe vitatu vya FA.
“Mipango yangu ni kutengeneza kikosi cha
kutetemesha, nilifanya hivyo wakati nilipoongoza timu hii kwa mara ya
kwanza na nataka kufanya hivyo kwa mara nyingine.”
No comments:
Post a Comment