MTOTO wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, John Nyerere, anatarajiwa
kuzikwa Jumatano hii kijijini kwao Mwitongo wilayani Butiama mkoani
Mara, baada ya kukamilika kwa taratibu za mazishi.
John alifariki juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alipokua
amelazwa baada ya kuugua maradhi ya mapafu na kisukari yaliyosababisha
kifo chake.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwao marehemu Msasani jijini
Dar es Salaam, mjukuu wa Mwalimu Nyerere, Moringe Magige, alisema mwili
wa marehemu John utaagwa leo Msasani kuanzia saa 7 mchana na baada ya
hapo utasafirishwa kesho kuelekea wilayani Butiama kwa mazishi.
“Baada ya kuwasili mwili saa 7 mchana kutakuwa na ibada maalumu ya
kumuombea marehemu itakayochukua muda wa saa moja,” alisema Moringe.
Aliongeza baada ya kumalizika kwa ibada, mtoto wa marehemu, Charles
Makongoro, atasoma wasifu wa marehemu na kwamba akimaliza watatoa
heshima ya mwisho.
Katika msiba huo viongozi mbalimbali wa chama na Serikali walihudhuria
kutoa rambirambi kwa familia ya Mwalimu Nyerere wakiongozwa na Waziri
Mkuu Mizengo Pinda pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Mkuu Pinda, alisema
wanashirikiana na familia katika msiba huo huku akiahidi kutoa taarifa
kwa viongozi wa nchi za Ukombozi wa Afrika ili nao waweze kujumuika
katika msiba huo.
Viongozi wengine waliohudhuria msiba huo ni pamoja na Rais mstaafu Ali
Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba, Makamu Mwenyekiti wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula na Katibu Mwenezi wa
chama hicho, Nape Nnauye.
No comments:
Post a Comment