Monday, 11 May 2015

TUKIMBIZANE NA KASI YA MAENDELEO '' ASEMA LOWASSA JANA AKIWA TABORA ''

 
Waziri Mkuu mstaafu na mbunge wa Monduli, Edward Lowassa amesema umefika wakati kwa Tanzania kukimbia kwa kasi ili kukabiliana na changamoto kubwa ya maendeleo ya sayansi duniani.

Akihutubia katika sherehe za jubilee ya miaka 25 ya uaskofu na 40 ya upadri ya Askofu Paul Ruzoka katika Jimbo Kuu Katoliki Tabora jana, Lowassa alisema maendeleo hayo yanapaswa yawe darasa la kuirejesha Tanzania katika falsafa ya elimu ya kujitegemea.
“Elimu ya kujitegemea inajenga misingi imara kwa wahitimu wanaomaliza shule  kuendelea na masomo, kujiajiri au kuajiriwa katika sekta mbalimbali,” alisema na kuongeza kuwa elimu ya Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi.

 
Lowassa alilipongeza Kanisa Katoliki kwa mchango mkubwa linaloutoa katika maendeleo  ya elimu nchini kwa kusaidia kupambana na ujinga, umaskini na maradhi.

Katika hatua nyingine, Lowassa aliliomba kanisa kushirikiana na Serikali na wananchi katika suala la ulinzi na usalama.
Lowassa alisema sasa kuna viashiria vya kuvurugika kwa amani, huku akikumbushia matukio ya kushambuliwa kwa nyumba za ibada visiwani Zanzibar na mkoani Arusha.
 “Jukumu la ulinzi ni letu sote, kwa hiyo kanisa nalo lina wajibu wa kuwakumbusha waumini wake kila wakati kutambua wajibu wa kila mmoja kuwa mlinzi wa ulinzi na usalama wa nchi.
“Baba Askofu ningependa pia kuchukua fursa hii kukuomba uendelee na juhudi za kuombea amani kwa ndugu zetu wa Burundi kwa kuwa hali ya huko  sasa imeanza kuchafuka,” alisema Lowassa.
Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Mhashamu Askofu Tarcius Ngalalakumtwa alisema Askofu Ruzoka amefanya kazi kubwa kuhakikisha amani inatamalaki nchini na nje ya nchi.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali  wakiwamo wabunge Profesa Athman Kapuya na Magreth Sitta.

No comments:

Post a Comment