KOCHA Mkuu wa Etoile du Sahel ya Tunisia, Faouzi Benzarti, ameingia
mitini baada ya kushindwa kutokea katika mkutano wa makocha na waandishi
wa habari ulioandaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili
ya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa leo katika
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Benzarti alishindwa kuhudhuria mkutano huo kwa madai walichoka baada
ya kuwa angani kwa saa tisa wakitokea Tunisia ambapo waliwasili Dar es
Salaam jana alfajiri.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto, Benzarti
aliwataarifu kwamba asingefika kwenye mkutano huo na kuwaomba radhi
kutokana na hilo.
Pamoja na kushindwa kutokea kwa kocha huyo, Kocha wa Yanga, Hans van
der Pluijm alisema amezikamata mbinu za Etoile du Sahel na atahakikisha
wanashinda mchezo huo wa raundi ya pili wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Mchezo huo utakaoanza 9:00 alasiri, Pluijm alisema amejiandaa
kikamilifu katika kuhakikisha wanashinda nyumbani ili waweze kujiweka
katika mazingira mazuri ya kusonga mbele watakaporudiana ugenini Mei
Mosi, mwaka huu.
Alisema anafahamu mbinu za wapinzani wao ambao mara nyingi wanapokuwa
ugenini wanafanya mashambulizi ya kushtukiza, huku wakilinda lango lao
ili wasifungwe mabao mengi.
Alisema atahakikisha wachezaji wake wanatibua mipango yao kwa
kuwalazimisha kufuata mfumo watakaocheza wao ili kuleta uwiano wa soka.
Alisema Eitole ni kati ya timu bora Afrika, lakini wataingia kwenye vita
na kushinda, hivyo mashabiki wanatakiwa kufika kwa wingi kuishangilia
timu yao.
Pluijm amewataka wachezaji wake kutofanya makosa ambayo yaliwasababishia
wang’olewe mapema na Al Ahly ya Misri katika michuano ya Ligi ya
Mabingwa msimu uliopita.
Alisema wachezaji wake walishindwa kuzitumia nafasi zaidi ya tano za
kufunga katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, ambao
walitolewa kwa penalti 4-3 baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1
mjini Alexandria.
Pluijm alisema kwa kulitambua hilo wachezaji wake hawatorudia makosa
kwani wanatakiwa kushinda kwa idadi kubwa ya mabao ambayo yatakuwa ni
mtaji kwao katika mchezo wa marudiano.
Alisema anaiheshimu Etoile du Sahel lakini wachezaji wake wamempa
matumaini ya kushinda, kutokana na nidhamu waliyoionyesha katika mazoezi
akiamini lolote linaweza kutokea ndani ya dakika tisini.
Alisema amewaandaa wachezaji wake kiufundi na kisaikolojia waweze
kujiamini na kupata matokeo mazuri katika uwanja wao wa nyumbani.
Katika mchezo huo, Pluijm anaweza kuwakosa Amisi Tambwe ambaye anaugua
malaria na Salum Telela aliyeumia kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania
Bara dhidi ya Mbeya City, uliochezwa wiki iliyopita katika Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Kikosi cha Yanga kinachotarajia kushuka uwanjani leo ni Ally Mustapha
‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin
Yondan, Mbuyu Twite, Hassan Dilunga, Mrisho Ngassa, Kpah Sherman na
Haruna Niyonzima.
Yanga wakiwatoa Etoile du Sahel wataingia katika hatua ya mtoano
wakiisubiri timu ambayo itashindwa kufuzu robo fainali ya Ligi ya
Mabingwa barani Afrika.
No comments:
Post a Comment