Wanasiasa wa Zanzibar wamegawanyika kuhusu hatua ya CCM kumfukuza uanachama mwanasiasa mkongwe, Hassan Nassor Moyo (pichani) baada ya kupatikana na hatia ya kuvunja miiko na maadili ya chama kwa kitendo chake cha kuhudhuria mikutano ya hadhara ya CUF na kutetea mfumo wa muundo wa Serikali tatu kinyume na sera ya chama chake.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti siku moja baada
ya mwanasiasa huyo kufukuzwa, baadhi ya wanasiasa walisema kuwa CCM
imefanya kosa kwa kutompa nafasi ya kujitetea juu ya tuhuma zilizokuwa
zinamkabili.
Aliyekuwa Kamishina wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Muhamad Yussuf Mshamba alisema kama Moyo alikuwa na makosa,
alitakiwa kuitwa kwenye vikao vya chama kuhojiwa kuhusu tuhuma
zilizokuwa zinamkabili katika ngazi zote badala ya kumtimua kibabe.
Alisema utaratibu uliotumika kumfukuza ni kinyume
na Katiba ya CCM pamoja na misingi ya demokrasia kwa vile amehukumiwa
bila ya kupewa nafasi ya kujitetea kwenye vikao ili kuhakikisha haki
inatendeka kabla ya kufanyika uamuzi.
“Mwanachama anapovunja miiko, maadili au kanuni za
chama uchunguzi peke yake hautoshi kutoa adhabu. Moyo alitakiwa kuitwa
na kujitetea kama kweli alifanya makosa kabla ya kufukuzwa,” alisema
Mshamba ambaye pia mwanadiplomasia mstaafu.
Naibu Katibu Mkuu wa ADC Zanzibar, Ali Makame Issa
alisema mambo yaliyomkuta Moyo ni ya kujitakia kwa sababu kila chama
kimeweka miiko, maadili na kanuni, hivyo mwanachama anapokwenda kinyume
lazima achukuliwe hatua.
“Vyama vya siasa vina utaratibu wake ukienda nje
ya utaratibu utapewa adhabu tu. Moyo alifika pahala unashindwa kumfahamu
kama ni CUF au CCM anatofautiana hadi na sera za chama chake,” alisema
Ali.
Alisema pamoja na CCM kuwa na wasemaji wake,
lakini Moyo alijigeuza msemaji wa CCM na kupinga misingi ya Mapinduzi na
Muungano wa Tanganyika bila ya kujali sera ya chama chake.
Kuhusu kupewa nafasi ya kujitetea, Katibu wa CCM
Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziza Mapuri alisema walikuwa wakimwandikia
barua za wito kwa ajili ya kuhojiwa na vikao kuanzia ngazi ya wilaya
hadi mkoa, lakini Moyo alikuwa akipiga chenga kuhudhuria.
“Kikao cha mwisho cha mkoa tulimwita kwa
kumuandikia barua kabla ya kumjadili na kumfukuza lakini baadaye
alitupigia simu na kutuambia yeye ni mtu mzima hawezi kuhangaika na
kutaka kikao kikafanyike nyumbani kwake lakini mikutano ya CUF na
makongamano anaudhuria Unguja na Pemba,” alisema Mapuri.
Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Mjini Unguja,
Baraka Shamte alisema Moyo amejichinja na kisu chake mwenyewe kwa sababu
alikuwa anafahamu vizuri kanuni, miiko na maadili ya chama chake kwa
sababu alishiriki kuzitunga baada ya kuzaliwa kwa CCM Februari 5, 1977.
“Moyo ameshiriki kutunga Katiba na kanuni za chama
lakini ameshindwa kuheshimu miiko na maadili na kuamua kujichinja na
kisu chake mwenye,” alisema.
No comments:
Post a Comment