Tuesday, 20 January 2015
ARSENAL YAONA TANZANIA !
KLABU ya Arsenal leo imeanza mazungumzo rasmi na makampuni 20 ya hapa nchini kwa lengo la kufungua mahusiano ya kibiashara lakini katika mpango huo makocha wa timu hiyo na baadhi ya nyota waliowahi kutamba watapata fursa ya kudhuru hapa nchini.
Mapema mwenyeji wa wageni hao, Afisa mtendaji mkuu wa EAG Group, Bw Imani Kajura, alisema hii ni fursa sahihi kwa makampuni ya Tanzania kuchangamkia ili kutambulika kimataifa, na kutoa fursa kwa Nchi, kunufaika na miradi ya kijamii itakayoendeshwa kwa ubia, endapo Arsenal itafanikiwa kupata wabia katika sekta ya biashara.
Akizungumza jijini leo, Mkurugenzi wa mahusiano ya kimaendeleo ya klabu hiyo Sam Stone amesema ujio wao nchini unalengo la kutaka kufungua milango ya kibiashara na baadhi ya makampuni makubwa na madogo nchini.
Mkurugenzi wa maendeleo na mahusiano wa klabu ya Arsenal ya England, inayoshiriki ligi kuu ya EPL, Sam Stone akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio wa uwekezaji wa klabu hiyo nchini, pamoja naye ni meneja wa kitengo hicho Daniel Willey.
Stone ambaye ameambatana na meneja wa kitengo hicho Daniel Willey amesema katika mpango huo pia Arsenal itawaleta nchini makocha wao wa soka la vijana kuja nchini kusaidia kukuza wachezaji vijana huku pia wachezaji wa zamani wa timu hiyo wakiwemo Thiery Henry,Robert Pires na Martin Keown wanaweza kuja nchini kutembelea miradi hiyo.
“Tutaanza kwanza kuzungumza na makampuni hayo ambayo yameonyesha kuhitaji kuonana nasi kati ya hayo wapo pia viongozi wa soka hapa nchini Tanzania,tumeona ni vyema tukaanzisha mahusiano haya baada ya kuona muamko wa Tanzania katika maeneo hayo,”alisema Stone.
“Tukikamilisha kila kitu kuhusu mahusiano haya wakati utekelezaji ukianza kuna uwezekano mkubwa wa makocha wetu wa vijana kuja hapa lakini pia wachezaji wetu wa zamani kama Pires,Henry na Keown wanaweza kuja hapa kama tulivyofanya nchi za Afrika Kusini, Uganda, Kenya, Misri.”
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment