Dodoma.
Uuzwaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) jana uliibua utata juu ya uhuru wa mihimili mitatu ya nchi baada ya wabunge kutaka kujadili suala hilo, huku Mwanasheria Mkuu wa Serikali akipinga.
Suala hilo liliibuka kwenye ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), ambayo iliitaka Serikali kutoa maelezo bungeni kama kweli hisa za Uda zimeuzwa kwa kampuni binafsi ya Simon Group Limited.
“Endapo hisa hazijauzwa, mchakato wa uuzaji wa hisa hizo utapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazohusika,” alisema mwenyekiti wa kamati hiyo, Rajab Mbarouk Mohamed wakati akiwasilisha taarifa hiyo ya mwaka ya LAAC.
Hata hivyo, alipomaliza kuzungumza, Spika Anne Makinda alilieleza Bunge kuwa amepokea taarifa mbili za kuwapo kwa kesi zinazohusu kampuni hiyo kongwe ya usafiri jijini Dar es Salaam na kutaka suala hilo lisijadiliwe.
Kauli yake iliungwa mkono na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, ambaye alisema ni kweli suala hilo lisijadiliwe kutokana na kesi hizo.
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alisimama na kueleza kuwa suala hilo lazima lijadiliwe, akisema Mahakama zisigeuzwe vichaka vya mafisadi. Hata hivyo, mjadala huo haukuendelea.
Taarifa ya LAAC iliibana Serikali kutaka ieleze zilipo Sh1 bilioni zilizochangwa na wadau wa mradi, zikiwamo manispaa za Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kuanzisha machinjio ya kisasa.
Uwekezaji huo wa manispaa za Jiji la Dar es Salaam ni katika mradi wa Kiwanda cha Nyama East African Meat Company Limited kilichopo eneo la Kiltex Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam.
Akizungumza bungeni jana jioni, mwenyekiti wa kamati hiyo, Rajab Mbarouk Mohammed alisema hayo wakati akisoma taarifa ya mwaka ya kamati yake kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30 mwaka jana.
Mbarouk alisema mwaka 2004 manispaa za Dar es Salaam na wabia wengine wawili, ambao ni Nicol ya Tanzania na Kampuni ya R&M ya Malaysia ziliingia makubaliano ya kuanzisha Kiwanda cha Machinjio ya Nyama kwa kuchangia Sh1.8 bilioni kama mtaji.
“Lakini mpaka sasa ni miaka 10 imepita kiwanda hicho hakipo na fedha hazipo,” alisema.
Alisema hiyo ni miongoni mwa baadhi ya mikataba ambayo LAAC imeibaini, isiyokuwa na tija bali hasara kwa halmashauri.
No comments:
Post a Comment