Chama cha riadha nchini Tanzania
(AT) kinakusudia kuwasilisha serikalini mkakati wa maandalizi wa miaka 6
kwa ajili ya michezo ya Olimpiki itakayofanyika Tokyo, Japan mwaka
2020.
Tanzania pia inakusudia kushiriki Olimpiki ya mwakani itakayofanyika huko Rio de Janeiro, Brazil katika michezo mbalimbali ikiwemo riadha, ngumi na kuogelea.
Tangu ianze kushiriki michezo ya Olimpiki ya majira ya joto mwaka 1964, Tanzania imeambulia medali mbili tu za fedha kupitia riadha huku michezo mingine ikishindwa kuambulia hata medali moja na kwa mujibu wa katibu mkuu wa AT, Suleiman Nyambui, lengo la mkakati huo ni kuwa na wakimbiaji vijana zaidi ya 100 watakaoandaliwa vizuri ili kuwa na mshiriki mzuri kama ilivyo Kenya, Ethiopia na nchi nyingine za Afrika.
Mkakati huo, pia utawahusisha wadau ili kuchangisha fedha na sehemu ya mkakati huo ni kuwapata wakimbiaji kutoka shule za msingi, sekondari na kupitia michuano ya Taifa.
Maandalizi duni yanayochangiwa na ukosefu wa fedha yamekuwa chanzo kikuu cha kufanya vibaya kwa wanamichezo wa Tanzania katika michuano mbalimbali ya kimataifa.
Serikali ya Tanzania, mwaka wa jana iliwapeleka zaidi ya wanamichezo 50 katika nchi za Afrika, Ulaya na Uchina kwa ajili ya kufanya mazoezi ya kujiandaa na michuano ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika huko Glasgow, Scotland ikiwa ni sehemu na mkakati wa kuwawezeza kushinda medali lakini ilishindikana.
Na kuepuka aibu kama hiyo, serikali imekuwa ikiviomba vyama kuwa na maandalizi ya muda mrefu badala ya maandalizi ya zimamoto yanayolitia aibu taifa hilo.
Kwa mujibu wa Nyambui, ili mwanariadha ashinde medali, anahitaji maandalizi yasiyopungua miaka 4 ili kuwa na ari ya kushinda ikiwa ni pamoja na ushiriki wa mara kwa mara katika michuano mbalimbali ya kimataifa.
No comments:
Post a Comment