MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe,
ameibuka tena na utata wa Sh bilioni 821 ambazo Serikali ya Tanzania
imelieleza Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kwamba imezitumia katika
mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Mradi huo unaogharimu dola za Marekani bilioni 1.55, kati yake asilimia
95 ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya China na asilimia 5
ni fedha zitakazotolewa na Serikali ya Tanzania.
Zitto ameibuka na utata huo zikiwa zimepita siku chache tangu
alipoonyesha wasiwasi juu ya matumizi makubwa ya fedha kwenye mradi huo
mwanzoni mwa mwezi huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa
wiki, Zitto alisema ripoti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(TPDC), iliyowasilishwa kwa kamati yake Novemba 3, mwaka jana,
inaonyesha kuwa fedha ambazo Tanzania ilikuwa imetoa ni dola za Marekani
31.3.
“Fedha ambazo Serikali imeahidi kutoa ni dola za Marekani 61.4, ambazo
tayari ilishatoa ni 31.3, lakini barua ya Tanzania (Letter of Intent)
kwenda IMF, inasema Serikali kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni mwaka
2014, ilitumia dola za Marekani milioni 464 (Sh bilioni 821), huu ni
utata, inabidi tupate majibu.
“Hata kwa hizi fedha za kutoka Exim Bank ya China ni mkopo ambao
unatakiwa ulipwe kati ya 2020 hadi 2040, sasa inakuwaje tena Serikali
inaonekana imezitumia fedha hizo kabla hata ya muda wa kulipa mkopo
haujafika?” alihoji Zitto.
Akifafanua kuhusu barua hiyo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),
Profesa Beno Ndulu, alisema mradi huo unagharimu dola za Marekani
bilioni 1.25 ambazo asilimia 95 ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki
ya Exim ya China.
Alisema dola za Marekani milioni 464 ambazo zimeelezwa kwenye barua hiyo ya IMF ni sehemu ya mkopo huo wa Benki ya Exim.
“Ile dola milioni 464 ni disbursement (malipo) ya Exim ya China, mkopo
wote ni dola za Marekani bilioni 1.25, kuna namna tatu ya kuripoti
madeni, namna ya kwanza, mwaka ule tulivyokubaliana inakuwa ni
commitment, kwamba mkopo ni dola bilioni 1.25, wale wakasema fedha ni
hizo na zitatumika kulipa ujenzi wa bomba, lakini hawatoi cash, wanalipa
makandarasi, wanalipa shughuli za ujenzi.
“Sasa disbursement ya ule mkopo inafanyika kadiri utekelezaji
unavyokwenda, kwa hiyo ile dola milioni 464 maana yake ni kiasi
kilichotolewa mwaka huo wa fedha 2013/14 kwa makandarasi katika shughuli
ya kujenga huo mradi, siyo kwamba fedha inatolewa inakuja hapa sisi
ndiyo tuwalipe makandarasi, inatolewa moja kwa moja kulingana na kazi
iliyofanyika, benki hiyo inatoa hiyo fedha kwa niaba yetu.
“Kwa kuwa ule mradi hautekelezeki kwa mwaka mmoja tu, ni wa karibu miaka
miwili, kadiri wanavyotekeleza ndivyo wanavyolipwa, kwa mikopo mingine
wewe unapewa hela kisha unawalipa makandarasi, lakini hii wanalipa
wenyewe, wanalipa kwa niaba yako, hii itaenda hadi fedha hiyo yote ya
mkopo iishe,” alisema Profesa Ndulu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, msimamizi wa mradi huo kutoka TPDC,
Mhandisi Kapuulya Musomba, alisema hadi sasa Serikali ya Tanzania
imeshalipa asilimia tano ya fedha hizo ambazo ilipaswa kuzitoa.
Mhandisi Musomba alisema sehemu ya fedha hizo ni dola za Marekani
milioni 31.3 zilizotumika kununua mashine (compressor) inayotumika
Songosongo.
Alisema fedha nyingine ni zaidi ya Sh bilioni 20 zilizotumika kwa kufidia watu waliopisha mradi huo na vitu vingine.
“Kwa sasa hivi hapa sina takwimu zozote, lakini ninachoweza kukwambia ni
kwamba ukijumlisha mambo yote, hiyo asilimia tano ya Serikali ni kama
dola za Marekani 94, na zote zilishatoka,” alisema.
No comments:
Post a Comment