Monday, 19 January 2015
MALI ZA JK KUPIGWA MNADA ....
Mali za Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba zimetangazwa kupigwa mnada kutokana na kushindwa kulipa deni analodaiwa na Benki ya CRDB.
Mali hizo zinahusisha eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 2,214 lililopo Mbezi Tangi Bovu, Dar es Salaam, kiwanja namba 1030 kilichosajiliwa kwa jina la John Damiano Komba na Salome Komba.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa kwenye vyombo vya habari, Kampuni ya Uwakili ya Mpoki & Associates Advocates inayoiwakilisha CRDB imetangaza kuuza eneo hilo la kibiashara lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya mafuta, maduka makubwa, benki, sehemu ya kufanyia mazoezi, hospitali na huduma nyingine za kijamii.
“Tayari eneo hilo lina nyumba kubwa ya kuishi upande unaotazamana na barabara mpya ya Bagamoyo. Kwa upande wa kusini mwa jengo kuu linalotazama barabara hiyo kuna nyumba nyingine ya kuishi, fremu za maduka na ofisi,” ilisomeka sehemu ya tangazo hilo.
Alipoulizwa juu ya gharama halisi anazodaiwa Kapteni Komba na muda wa deni hilo, mmiliki wa Kampuni ya Mpoki & Associates Advocates inayoratibu mnada huo, Mpale Mpoki alisema maelezo yote yanayohusu kiasi cha mkopo na muda wa deni yatajibiwa na CRDB wenyewe.
Hata hivyo, uongozi wa CRDB haukupatikana jana kuzungumzia suala hilo na Kapteni Komba alipoulizwa alisema hakuna jambo kama hilo... “Hakuna kitu kama hicho, waulize hao waliotoa hilo tangazo.”
(SOURCE) MWANANCHI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment