Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia, mshirika wa muda mrefu wa Marekani katika mapambano dhidi ya ugaidi na wenye msimamo mkali wa ki-Islam amefariki. Inaaminika alikuwa na umri wa miaka 90 na alikuwa mgonjwa kwa muda mrefu.
Kaka yake wa kambo Prince Salman atarithi ufalme nchini humo. Salman anakisiwa kuwa na umri wa miaka 79 amekuwa mwana mfalme na waziri wa ulinzi tangu mwaka 2012.
Wakati huo huo Rais Barack Obama alitoa rambi rambi zake binafsi na pole za watu wa Marekani kwenda kwa watu wa Saudi Arabia pamoja na familia ya kifalme. Bwana Obama alisema mfalme huyo wakati wote alikuwa muwazi na alikuwa shujaa kwa vitendo vyake ikiwemo kutumia uhusiano wa Marekani na Saudi Arabia kama nguvu ya usalama na uthabiti.
Mfalme Abdulla alitawazwa rasmi kuwa mfalme mwaka 2006. Lakini alikuwa akitawala tangu mwaka 1995 wakati mtangulizi wake na kaka wa kambo, mfalme Fahd alipopata kiharusi.
Abdullah inaaminika kuwa alizaliwa mjini Riyadh mwaka 1924 kutoka familia ya ki-Conservative ambapo mila na tamaduni za kiislamu zilisisitizwa. Wakati akikua kuingia ujana, mafuta yaligunduliwa katika jangwa la Saudi Arabia na nchi hiyo ilinyanyuka kuwa muuzaji wa juu duniani wa mafuta na kupelekea utajiri wa haraka kwa familia ya kifalme. Hadi anachukua udhibiti, Abdullah alianza harakati za mabadiliko ya kisasa katika ufalme.
Wanawake walipewa sauti katika siasa na waliruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi wa ndani kwa mara ya kwanza mwaka huu. Pia aliimarisha vyuo vikuu vyenye muundo wa magharibi ambapo wanafunzi wa jinsia zote walichanganyika na kusoma pamoja darasani. Muziki uliopigwa marufuku hapo awali ulisikika kwenye televisheni na redio za Saudi Arabia.
Mfalme Abdullah alikuwa jasiri katika sera zake za mambo ya nje . Alipendekeza makubaliano ya amani ambapo mataifa wanachama wa Arab League wataitambua Israel kama wa-Palestina wanapata taifa lao wenyewe. Katika taarifa ya kidiplomasia iliyovuja Marekani, mfalme Abdullah alisihi jeshi la Marekani kuishambulia Iran na “kukata kichwa cha nyoka” ili kusitisha nchi hiyo kuendelea na uzalishaji wa silaha za nyuklia.
Saudi Arabia ni moja ya wasambazaji wakubwa wa silaha kwenda kwa waasi wanaopigana kuiangusha serikali ya Syria. Ni mwanachama anayeongoza ushirika unao-ongozwa na Marekani katika mapambano dhidi ya kundi la Islamic State nchini Irak na Syria. Saudi Arabia ni sehemu ya muungano wa kiuchumi wa G20 na taasisi ya biashara duniani. Licha ya mageuzi nyumbani na ya wastani nje ya nchi makundi ya haki za binadamu yanaendelea kuinyooshea kidole Saudi Arabia. Wanasema wanawake bado wananyimwa haki nyingi za msingi.
Mfalme huyo alikataa kuunga mkono harakati za mapinduzi ya kiarabu maarufu “Arab Spring” ambayo yaliwaondoa madarakani madiktekta nchini Tunisia, Misri, Libya na Yemen.
No comments:
Post a Comment