Tuesday, 31 March 2015

BALOZI AIPA YANGA MAUJANJA YA PLATINUM ... >>

Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Adadi Rajabu amesema wapinzani wa Yanga katika Kombe la Shirikisho Afrika, FC Platinum sasa wanafanya mbinu zote usiku na mchana kuhakikisha wanashinda mchezo huo wa marudiano.
                              
Balozi Rajabu yuko jijini Arusha akishiriki kongamano la tatu la viongozi vijana barani Afrika linalowashirikisha zaidi vijana 400 kutoka nchi za Afrika na China lililofunguliwa juzi na Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe.

Akizungumza na gazeti hili jana, balozi Rajabu alisema kipigo cha mabao 5-1 ilichopata Platinum kimewaacha midomo wazi Wazimbambwe kutokana na ubora wa timu hiyo.

Alisema nchi hiyo kwa sasa inajadili kipigo hicho na taarifa alizonazo kwa sasa, FC Platinum kwa kushirikiana na Serikali ya Zimbabwe inatengeneza mazingira ya kuhakikisha mchezo wa marudiano Yanga wanafungwa.
“Kipigo cha Yanga kule Zimbabwe wanakiita janga na wengi hawaamini, hivyo wamejipanga kuhakikisha wanarudisha heshima yao kwa kushinda mchezo huo wa marudiano,” alisema balozi huyo.

Aliongeza kuwa amepata taarifa kuwa washambuliaji wawili wa Platinum hawakucheza mechi ya kwanza kutokana na kuwa majeruhi, lakini kwa sasa wamerejea kikosini na wako kambini wanajifua.

“Kocha wa FC Platinum, Norman Mapeza ni miongoni mwa watu wa heshima na wanaoaminiwa na serikali, hata yeye amekuwa akisugua kichwa kuhakikisha anajenga heshima yake katika mchezo wa marudiano,” alisema Balozi Rajabu.

Kocha Yanga ajigamba

Kocha wa Yanga, Hans Pluijm amesema timu yake ina uwezo wa kupambana na klabu yoyote Afrika na itashangaza kwenye Kombe la Shirikisho inaloshiriki.

Kabla ya hapo, Yanga iliiondoa BDF X1 ya Botswana na kama ikiiondosha Platinum itakutana na mshindi kati ya Etoile du Sahel ya Tunisia au Benfica de Luanda ya Angola.
Pluijm alisema ana uzoefu na mashindano ya Afrika na anaamini ana kikosi bora kitakachoshangaza wengi katika mashindano ya mwaka huu.

“Sasa hivi tunajiandaa na mchezo wa marudiano dhidi ya Platinum, niseme tu kuwa ni kama tumevuka nusu na tunakwenda kumaliza kazi Zimbabwe, na naamini tutashinda mechi hiyo.

No comments:

Post a Comment