Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Masheikh na wanazuoni wa Kiislamu, Sheikh Khamis Mataka akizungumza jijini Dar es Salaam jana kuhusu msimamo wa taasisi hiyo kuhusu Mahakama ya Kadhi, kuli ni Sheikh Mohamed Idd
Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania imejibu hoja zilizotolewa wiki iliyopita na Jukwaa la Wakristo nchini kuhusu Katiba Inayopendekezwa, Mahakama ya Kadhi na hali ya usalama na amani ya nchi.
Machi 10, mwaka huu maaskofu kupitia Jukwaa la Wakristo Tanzania walitoa tamko na kuwataka waumini wao kuipigia kura ya hapana, Katiba Inayopendekezwa kwa sababu imepatikana kwa njia za hila na kibabe, jambo ambalo sasa limesababisha mvutano.
Katika tamko hilo lililosainiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcicius Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet, maaskofu hao walisema uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi ni uvunjifu wa Katiba na kuwa unahatarisha amani ya nchi.
Walisisitiza kuwa Serikali ikiruhusu masuala ya kidini kuingizwa kwenye mfumo wa sheria yatasababisha migongano kati ya pande pindi zinazotofautiana.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni, Sheikh Khamis Mataka alisema maaskofu wamejisahau kwamba wao ni viongozi wa kiroho na kuwa wana wajibu wa kumpokea mtu yeyote na kumpa neno la hekima bila kujali tofauti zao na siyo kushinikiza jambo.
Alisema Watanzania wapatiwe Katiba Inayopendekezwa, wapate elimu, waisome kwa makini na kuielewa ili wawe na uwezo na uhuru wa kuamua kupiga kura ya ‘Ndiyo’ au ‘Hapana’ bila shinikizo lolote kutoka kwa viongozi wa dini.
“Maaskofu wamefanya kosa kubwa kuwachagulia waumini wao aina gani ya kura wanayopaswa kupiga. Hiyo siyo kazi yao, wao wajikite katika kuhimiza watu kujitokeza kupiga kura au kutoa elimu, siyo kuwaambia wapige kura ya ‘Hapana’. Hilo ni suala la mtu binafsi kadri anavyolielewa jambo husika,” alisema.
Sheikh Mataka alibainisha kuwa Mahakama ya Kadhi inayolalamikiwa na Jukwaa la Wakristo ni haki ya Waislamu na haiwahusu wala haihitaji ridhaa ya wasiokuwa Waislamu kama ambavyo wao hawaingilii baadhi ya mambo ambayo Serikali inawafanyia Wakristo.
Alisema Mahakama ya Kadhi inatambuliwa katika sheria za Tanzania kwa sababu ni moja wa vyanzo vya sheria ya Tanzania. Alisema sheria hizo zimekuwa zikitumika kuhukumu kesi za Waislamu kuhusu ndoa, talaka na mirathi.
“Tangu mwaka 1963 ilipopitishwa Sheria ya Mahakama za Mahakimu (Magistrate Courts Act 1964), ikifuatiwa na Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu ya 1964 na kuhitimishwa na Sheria ya Ndoa ya 1971, Mahakama ya Kadhi inatambuliwa kisheria. Si kweli kwamba tutavunja Katiba,” alisema Sheikh Mataka. Alisisitiza kuwa mahakimu waliokuwa wanasikiliza kesi hizo hawana ujuzi wa dini ya Kiislamu, hivyo wanachokitaka sasa ni Waislamu wenyewe kuamua kesi zinazowahusu kwa kuwa wana ujuzi wa masuala hayo. Kiongozi huyo ameitaka Serikali ipuuzie tamko la maaskofu na iendelee na mchakato wa Mahakama ya Kadhi. Pia, aliwataka maaskofu wawe watulivu na kuwa Serikali ni ya Watanzania wote.
“Maaskofu wameamua kuanzisha utamaduni mpya wa kuyaendea mambo ya kisiasa kwa misingi ya kiimani. Hilo ni tishio la kuwagawa Watanzania kwa misingi hiyo,” alisema Sheikh Mataka na kuongeza kuwa madai kwamba Waislamu walipewa rushwa ni dharau na kutowaheshimu, jambo ambalo lina athari zake.
Sheikh Mataka aliongeza kuwa jukumu la ulinzi na usalama wa Taifa ni wajibu wa kila mwananchi na kuwa si busara kulilaumu Jeshi la Polisi kutokana na vitendo vya kigaidi na mauaji ya albino yanayotokea nchini.
No comments:
Post a Comment