Tuesday, 17 March 2015

HALI YA KISIASA BURUNDI ... UN YALAANI SHAMBULIO LA AGATHON RWASA >>

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa wito kwa serikali ya Burundi kufanya " uchunguzi wa kina" ili kuwapata na kuwafungulia mashtaka wahusika wa shambulio dhidi ya mke wa Kiongozi wa kihistoria wa chama cha Fnl, ambaye pia ni mwanasiasa wa upinzani Agathon Rwasa.

Ban Ki Moon ameelezea wasiwasi wake kuhusiana na shambulio hilo la siku ya Jumapili ambalo, kwa mujibu wa Ban, linatishia kuongeza mvutano nchini humo miezi mitatu kabla ya uchaguzi wa Rais.

Naibu msemaji wa katibu mkuu huyo, Farhan Haq amesema kuwa Ban anaitaka serikali ya Burundi haraka iwezekanavyo kufanya uchunguzi wa kina katika tukio hilo na kuviomba vyama vyote vya siasa nchini Burundi kulaani aina zote za ghasia za kisiasa na uchochezi wa chuki au vurugu.

Siku ya Jumapili, Annonciate Haberisoni amejeruhiwa kichwani baada ya kukoswa na risasi alizorushiwa na mtu asiyejulikana mtaa wa Asiatique (uarabuni) mjini Bujumbura akiwa katika saluni moja kusuka nywele.

Mvutano nchini Burundi unaendelea kuongezeka katika muktadha wa suala tata la uwezekano wa rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kuwania awamu ya tatu ya urais kinyume na Katiba ya nchi hiyo, huku Agathon Rwasa akionekana kuwa mmoja wa wapinzani wakuu katika kinyanganyiro hicho.

No comments:

Post a Comment