Thursday, 19 March 2015

RAIS KIKWETE ASEMA AKISISITIZA JUU YA MKATABA WA ARUSHA ...>>

Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, awasihi wanasiasa wa Burundi kuheshimu Mkataba wa Arusha na Katiba ya Burundi. 

Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye anahitimisha ziara yake ya siku mbili mjini Bujumbura, nchini Burundi, amewatolea wito wanasiasa wa Burundi kuheshimu mihula ya kuwa madarakani kulingana na Mkataba wa Arusha na katiba ya Burundi.
 
Wito huo wa Rais Kikwete unakuja wakati ambapo joto la kisiasa likiendelea kupanda siku baada ya siku nchini Burundi.
Hayo yanajiri wakati mashambulizi dhidi ya wanasiasa na familia zao yakianza kushuhudiwa. Hivi karibuni mke wa kiongozi wa kihistoria wa chama cha Fnl, ambaye pia ni mwansiasa wa upinzani, Agathon Rwasa, alijeruhiwa kwa risasi baada ya mtu asiyojulikana kumshambulia akiwa salooni, mjini kati Bujumbura.
 
Rais Kikwete amewasihi wanasiasa wa Burundi kuweka kando tofauti zao na kuheshimu Mkataba wa Arusha pamoja na Katiba ya nchi.
 
Wito huo wa Kikwete unatolewa baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kumuonya Rais Pierre Nkurunziza kutogombea muhula wa tatu kwa kuhofia kulipuka kwa machafuko.

Hata hivyo Rais Pierre Nkurunziza hajasema iwapo atagombea au la, lakini amekuaa akionesha nia ya kugombea kwa muhula wa tatu. Hivi karibuni kiongozi wa chama tawala cha Cndd-Fdd, Pascal Nyabenda alieleza wazi kwamba kama rais Nkurunziza hatogombea kuna hatari chama hicho kishindwe uchaguzi.

Kauli hii ya Pascal Nyabenda ilizua mvutano kati yake na msemaji wa chama cha Cndd-Fdd, Onésime Nduwimana, ambaye alikanusha madai hayo ya Pascal Nyabenda huku akibaini kwamba chama cha Cndd-Fdd kina wagombea wengi, mbali na Pierre Nkurunziza.

No comments:

Post a Comment