Watu wasiojulikana wamemteka Muuguzi wa Hospitali ya Mwananyamala, Pili Amiri, huku wakitoa sharti la kupewa Sh5 milioni ili wamuache huru.
Pili, mwenye umri wa miaka 26, alitekwa akiwa
nyumbani kwake maeneo ya Mwananyamala Komakoma, saa tano asubuhi,
Alhamisi wiki iliyopita na kuingizwa katika gari linalodaiwa kuwa ni la
watekaji hao.
Akizungumzia tukio hilo, mjomba wa Pili, Rahim
Kangile alisema watekaji hao baada ya kumteka walipiga simu kwa kutumia
namba ya Pili wakidai kutumiwa kiasi hicho cha fedha.
“Waliposema wanataka Sh3 milioni, ili wamuache,
tuliwatumia lakini hawakufanya hivyo hadi jana, wakasema tuwatumie tena
Sh2 milioni, tumetuma leo(jana) lakini mpaka sasa hakuna chochote
tulichofanikiwa,” alisema.
Kangile alisema watekaji hao walitoa vitisho kuwa
endapo malipo hayo hayatafanyika basi watafanya jambo lolote baya kwa
muuguzi huyo.
“Tulipoona wanatoa vitisho tuliwatumia hizo hela lakini hawajafanya chochote la kuonyesha watamuachia Pili,”alisema.
Alisema watekaji hao walitaka fedha zitumwe katika
akaunti ya NMB ya Pili, jambo ambalo lilitekelezwa na baadaye
ikabainika kuwa miamala kadhaa imefanywa kupitia mtandao wa ATM kutoka
kwenye akaunti ya muuguzi huyo.
Akizungumzia iwapo Pili alikuwa na maadui, Kangile
alisema hawana chembe ya shaka kama muuguzi huyo alikuwa na ugomvi na
watu hadi kufikia hatua ya kumteka.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk
Sophiniasis Ngonyani alisema Pili hakutekwa akiwa mazingira ya
hospitali, bali akiwa nyumbani kwake na kueleza kuwa wanafamilia
wametakiwa kutoa kiasi hicho cha fedha ili aachiwe huru.
“Ni kweli huyu muuguzi wetu ametekwa tangu
Alhamisi iliyopita, tumezipata taarifa kutoka kwa ndugu zake, baada ya
kutokuonekana nyumbani kwa siku kadhaa,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa mjomba wa wanafamilia, siku
moja baada ya watekaji kumteka msichana huyo, walipiga simu wakitaka
kupewa kiasi cha Sh3 milioni.
Dk Ngonyani alisema polisi wameshapewa taarifa za tukio hilo na wanaendelea kufanya kazi yao ili kupata taarifa za ndani zaidi.
No comments:
Post a Comment