Tuesday, 31 March 2015

MTANZANIA AKAMATWA KWA UGAIDI KENYA ..>>

Vyombo vya usalama nchini Kenya, vinawashikilia wasichana watatu akiwamo Mtanzania, kwa kile kunachodaiwa kutaka kujiunga na kundi la kigaidi la al-Shabaab huko Somalia.
                               
Taarifa kutoka kwa Kamishna wa Polisi Jimbo la El -Wak, mpakani mwa Kenya na Somalia, Nelson Marwa amesema Mtanzania aliyekamatwa, alijieleza kuwa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika, Sudan.

 Mtanzania huyo, Ummul-Khayr Sadir Abdul (19), mwenyeji wa Zanzibar, anatajwa kuwa kiongozi wa kundi hilo lililopanga kujiunga na al-Shabaab.

 Wasichana wengine waliokamatwa pamoja na Ummul-Khayr, ni Maryam Said Aboud na Khadija Abubakar Abdulkadir wote raia wa Kenya.

“Hawa wasichana watatu, inaaminika kuwa walikuwa wanakwenda Somalia kupata mafunzo ya kigaidi na baadaye kufanya mashambulizi ya kujitoa mhanga,” alisema Kamishna Marwa.

Akizungumzia suala hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, DCI Diwani Athumani alisema: “Tunafuatilia hatujapokea taarifa zaidi ya hizo.”

Kamishna Marwa alisema raia hao  wawili wa Kenya, mmoja  ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya kilichopo Thika, Jimbo Kiambu na mwingine ni mwanafunzi wa Sekondari ya Burhania, iliyopo Malindi, Kilifi.

“Serikali imepata taarifa kuhusu watu wanaokusanya watu kutoka Afrika Mashariki ili wakajiunge na makundi ya  ugaidi nchini Somalia, wakala wetu wa usalama wamepata taarifa hizo na kufanikisha kukamatwa kwa wasichana hao,” alisema Kamishana Marwa.

Hivi karibuni, tovuti ya al-Jazeera ilitoa taarifa za kukamatwa kwa mkanda wa video ulioonyesha mwakilishi wa kundi la kigaidi la Dola ya Kiislamu ya Iraq na Levant (ISIL) akimtaka kiongozi wa kundi la al-Shabaab kuliimarisha kwa kufanya mashambulizi ya kigaidi katika miji ya  Mwanza na Dar es Salaam.

 Kamishna Marwa alisema ingawa nyaraka za wasichana hao zote zinaonyesha kuwa ni wanafunzi, lakini bado walibanwa  kwa maswali kuhusu sababu inayowapeleka nchini Somalia.

Aliongeza zaidi kuwa chanzo cha habari cha kiusalama kilieleza kuwa nyaraka za wasichana hao zilionyesha kuwa walikuwa wakienda kuolewa na wanajeshi wa kundi la al-Shabaab.

No comments:

Post a Comment