Bondia Mohamed Matumla Junior atapanda ulingoni leo kumvaa Mchina, Wang Xiu Hua katika pambano la kuwania ubingwa wa Super Bantam wa WBF Eliminator kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Matumla Jr, ambaye ni mtoto wa bingwa wa zamani wa WBU, Rashid Matumla ‘Snake Man’ alisema jana kuwa hawezi kuwaangusha Watanzania.
“Niko vizuri, sitawaangusha Watanzania kesho (leo), niwaombe wajitokeze kwa wingi kuniunga mkono,” alisema.
“Hatamaliza raundi na endapo akimaliza, basi yeye ni kidume, nitampiga na kumwondoa mapema ulingoni, naomba mashabiki na wapenzi wa ngumi waje waone vitu vyangu nilivyorithishwa na baba pia kocha wangu (Rashid Matumla),” alisema bondia huyo chipukizi.
Akizungumza wakati wa kupima uzito mabondia hao, bingwa wa zamani wa dunia, Francois Botha alisema kuwa anaamini kila bondia amejiandaa vizuri katika pambano hilo na kumtaka kila mmoja kutumia mbinu alizojifunza wakati wa maandalizi.
Botha alisema kuwa bingwa wa mchezo huo atakuwa amekata tiketi ya kupigana katika ngumi za utangulizi kwenye pambano la dunia, kati ya Floyd Mayweather Junior wa Marekani na Manny Pacquiao wa Ufilipino, Mei 2 jijini Las Vegas, Marekani.
No comments:
Post a Comment