Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imetangaza katika tovuti yake majina 287 ya washtakiwa waliopatikana na hatia katika kesi za rushwa.
Miongoni mwa majina yaliyotangazwa kupitia tovuti
yake www.pccb.go.tz wamo wafanyabiashara, wanasiasa, waandishi wa
habari, walimu, wauguzi, polisi, mwanafunzi na watumishi mbalimbali wa
umma.
Hatua hiyo ya Takukuru ni mwanzo wa mfumo na
utaratibu mpya ulioanzishwa na taasisi hiyo wa kuwatangaza hadharani
washtakiwa wote waliopatikana na hatia katika kesi zinazohusu rushwa.
Ofisa Uhusiano wa taasisi hiyo, Doreen Kapwani
alisema jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa, utaratibu
huo ambao umeanza kutumika Machi mwaka huu ni sehemu ya utekelezaji wa
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Alisema utaratibu huo utasaidia kuwahabarisha
wananchi kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuwashughulikia
wala rushwa.
“Kutokana na utaratibu huo, majina, taarifa
binafsi, maelezo ya mashtaka ya watu waliopatikana na hatia, yatakuwa
yanapatikana katika tovuti ya taasisi katika sehemu yenye kichwa cha
habari ‘Wahalifu wa Makosa ya Rushwa’,” alisema Kapwani.
Hata hivyo, Kapwani alitoa angalizo kuwa taarifa
zinazowekwa hadharani ni zile tu za washtakiwa ambao walifunguliwa
mashtaka dhidi ya rushwa na kesi zao kutolewa hukumu na Mahakama.
Akizungunzia kuhusiana na hatua hiyo, Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali linalojihusisha na Masuala
ya Kijamii (Fordia), Buberwa Kaiza alisema hiyo ni hatua nzuri lakini
haoni kama itasaidia.
“Tanzania ilipofikia karibu kila mtu ni mla
rushwa. Mbaya zaidi kuna rushwa kubwa ambazo Takukuru imesema haiwezi
kushughulika nazo... sina imani na hatua hiyo,” alisema Kaiza na
kuongeza kuwa wanafanya hivyo ili kujionyesha kuwa wanafanya kazi.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema: “Sidhani kama utaratibu huo
utasaidia kwa sababu kuna watu hata majina yao yakichapishwa hadharani
hawatajali.”
Alisema kama mtu anatoa au kupokea rushwa tayari
hana hofu yoyote, hivyo hata jina lake likichapishwa hataona shida wala
kuhofia.
“Rushwa ni suala kubwa. Jambo la muhimu ni kuanza
kulishughulikia tatizo hilo kwa upande wa maadili. Tutafute namna na
kurudisha maadili… watu wawe na maadili. Huo ndiyo utakuwa mwanzo mzuri
wa kupambana na rushwa,” alisema.
No comments:
Post a Comment