Ngorongoro. Ahadi ya chakula iliyotolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa jamii ya wafugaji wa Kimasai, juzi iliharibu mkutano wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana baada ya vilio vya wazee kutawala mkutanoni na kumlazimu kiongozi huyo kuamuru uahirishwe hadi majibu yapatikane.
Wananchi hao walianza kumlilia Kinana wakisema Serikali imewadanganya na kuwafanya waishi maisha yasiyo na matumaini.
Katika mkutano huo uliofanyika Kijiji cha
Nainokanoka, Kinana alijikuta akishindwa kujibu maswali ya wananchi,
yote yakielekea kwa Waziri Mkuu kuhusu ahadi yake ya kuwapatia chakula.
Wengi wa wananchi hao walionekana kuishutumu Serikali na hasa Ofisi ya Waziri Mkuu wakisema imekuwa ikiwadanganya kila wakati.
Mbunge wa Ngorongoro ambaye pia ni Naibu Waziri wa
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Kaika Telele ndiye aliyefungua njia
akisema kuwa baada ya Serikali kuwazuia wananchi wasilime mazao ya
chakula, Waziri Mkuu alitoa ahadi ya kuwapatia magunia 10 ya nafaka kila
kaya kwa mwaka lakini utekelezaji wake ni wa kusuasua.
Mmoja wa wanakijiji hao, Sinati Kahombo ndiye
aliyeanza kuwaliza wenzake alipopanda jukwaani na kumuomba Kinana aeleze
ni kosa gani Wamasai walimkosea Mungu ambalo halisameheki.
“Napiga magoti kuomba msamaha kwa Serikali ili
tusamehewe, njaa imewakimbiza watoto wetu vijana ambao wanafanya kazi ya
kulinda majumba ya walionacho lakini cha ajabu tunarudishiwa miili tu,
watu wote hapa unatuona kama umri tunalingana ni kutokana na njaa,”
alisema huku akiangua kilio kilichoitikiwa na wengi.
Kahombo aliishangaa Serikali kuwazuia kulima
bustani ndogo katika maeneo yao huku ikiruhusu hoteli kubwa kujengwa
katika korido za wanyama ndani ya hifadhi.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nainokanoka, Edward Ngunyi alisema hali ni mbaya katika kata yake yenye wakazi wapatao 15,420.
Ngunyi alisema kabla ya kuzuiwa kulima, wananchi
wa kata yake walikuwa wakijishughulisha na kilimo cha viazi katika
mashamba madogo ambayo yalisaidia kuwainua kiuchumi.
“Nimewasikia, nimewaelewa poleni sana ndugu zangu,
nikitaka kuahidi nitakuwa mwongo pia, bali ahadi yangu ni hii, ndani ya
mwezi mmoja nitakuja na mawaziri wote husika kwenye uwanja huu ili
tuzungumze,” alisema Kinana.
Katibu huyo alisema atawaomba katibu mkuu wa
Maliasili na Utalii, waziri anayeshughulikia maafa (Jenister Mhagama) na
waziri yeyote ambaye waziri mkuu ataona inafaa aambatane naye
kuzungumza nao.
No comments:
Post a Comment