Tuesday, 31 March 2015

YA GWAJIMA .. NA MBWE MBWE ..!

 

SIKU chache baada ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kukamatwa na kuhojiwa na polisi na hatimaye kuzimia, utata mpya umeibuka juu ya kiongozi huyo wa kiroho.
 

Utata huo unahusu uraia, historia yake, utajiri na umiliki wa silaha ambayo Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linadai haina kibali huku yeye akidai ana vibali vyote.
 

Hali hiyo imeibuka huku nyuma ya pazia kukiwa na sintofahamu juu ya hatima yake.
Ingawa Askofu Gwajima, amelazwa Hospitali ya TMJ kwa siku ya tano leo, bado anaendelea kushikiliwa na polisi kwa tuhuma za kutoa lugha chafu dhidi ya Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.


AHOJIWA KWA STAILI YA FBI

Baada ya kujisalimisha polisi Machi 27, mwaka huu, Askofu Gwajima anadaiwa kuhojiwa kwa staili ya Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).
Inaelezwa alihojiwa na makachero tofauti waliokuwa wakipishana katika chumba cha mahojiano na ambao wanaonekana kubobea katika taaluma hiyo.
Wakati akidhani mahojiano yamemalizika, inadaiwa waliingia maofisa wengine kumhoji maswali tofauti tofauti, mtindo ambao unatumiwa zaidi na wapelelezi wa FBI.
Hatua hiyo, pia inadaiwa kuchangia kuzimia kwake ambapo awali alidhani mahojiano yangekuwa ni kuhusu kumkashifu Kardinali Pengo tu.


KULAZWA HOSPITALI

Kabla ya kulazwa katika Hospitali ya TMJ, Askofu Gwajima alipelekwa katika Hospitali ya Polisi Kurasini na baadaye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambapo yeye na wafuasi wake waligoma na kutaka atibiwe TMJ ambapo kuna daktari wake maalumu.

URAFIKI NA WANASIASA
 

Askofu Gwajima, kwa muda sasa amekuwa rafiki wa wanasiasa mbalimbali nchini wakiwamo wa vyama vya upinzani, chama tawala, wastaafu pamoja na baadhi ya mawaziri walioko ndani ya Serikali ambao hukutana faragha, hadharani na wengine hushiriki katika ibada kanisani kwake.
Baadhi ya wanasiasa wa upinzani tayari wamemtembelea hospitalini alikolazwa.


UTATA SAKATA LA DK. ULIMBOKA
 

Sura ya pili ya Askofu Gwajima, ilianza kuonekana mwaka 2012, baada ya kanisa lake kuingia katika utata na sintofahamu baada ya kijana aliyedaiwa kumteka na kumtesa, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka kukamatwa na polisi.
 

Polisi walimkamata kijana huyo kwa kile kilichodaiwa kujisalimisha kwenye kanisa la Askofu Gwajima ambalo alikwenda kutubu kosa la kumshambulia Dk. Ulimboka.
 

Mtuhumiwa huyo, Joshua Mlundi, raia wa Kenya alikiri kuhusika kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka akiwa na wenzake 12 waliokodiwa na mtu aliyehisi anatoka serikalini.
 

Hata hivyo, Askofu Gwajima alisema Mlundi hakwenda kanisani hapo kutubu, bali alitaka kumuona kiongozi huyo wa kiroho baada ya kumweleza kuwa alikuwa na tatizo la kuropoka.

MAISHA YA KITAJIRI

Askofu Gwajima ni kiongozi wa kiroho mwenye ukwasi pengine kuliko wote nchini.
 

Anadaiwa anamiliki helikopta yake mwenyewe, gari la kifahari aina ya Hummer lenye thamani ya Sh milioni 250 na nyumba ya ghorofa nne maeneo ya Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.
 

Pamoja na kumiliki vitu hivyo, Askofu Gwajima amewanunulia wachungaji wake magari 30, kila mmoja gari zuri la kutembelea wakati wa kueneza injili.
Pia, amewanunulia waumini wake mabasi 20 ya kuwapeleka kanisani na kuwarudisha makwao siku za ibada na wakati wa maombi maalumu.
 

Pia anamiliki shamba la mifugo wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Katika kanisa lake, Askofu Gwajima amefunga spika maalumu zenye nembo ya ‘JG’ yaani Josephat Gwajima ambazo amezinunua nchini Marekani kwa oda maalumu.


KAULI TATA ZA GWAJIMA

Mwaka jana wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Dengue, Askofu Gwajima alikaririwa akisema hakuna ugonjwa kama huo isipokuwa umetengenezwa ili watu wajipatie fungu kutoka serikalini.
 

Alisema mbu aina ya Ades anayeeneza ugonjwa huo, alikuwapo tangu siku nyingi lakini hakuwa na madhara hadi baadhi ya viongozi ambao hakuwataja walipoutangaza na kuwalipa watu ili watangaze wameambukizwa ugonjwa huo.

URAIA NA HISTORIA YAKE

Suala la uraia wa Askofu Gwajima limekuwa mjadala kwa baadhi ya Watanzania, wakionyesha shauku ya kutaka kujua historia ya maisha yake.
Vyanzo mbalimbali ikiwamo mitandao ya kijamiii ya ‘twitter’, ‘facebook’ na tovuti yake, vimebainisha kuwapo kwa sintofahamu nyingi kuhusu asili yake.
 

Katika tovuti yake, Askofu Gwajima ambaye alianzisha kanisa lake mwaka 1994, hakutaja jina la kijiji alichozaliwa ingawa anasema alizaliwa mwaka 1970 mkoani Mwanza.
 

Katika tovuti yake hiyo, ameelezea historia yake akisema ni mtoto wa 12 katika familia yao ambayo iliishi katika kijiji ambacho hakikuwa na kanisa.
 

Anasema katika tovuti yake kuwa alipatwa na maradhi ya kupooza akiwa na umri wa miaka 10.
 

Alitaja sababu iliyosababisha apooze kuwa ni ajali ambayo hakuibainisha ni ya aina gani, ingawa anasema alikaa kitandani kwa muda wa miaka sita na kupoteza matumaini ya kupona.
 

Hali hiyo, anaelezea ilisababisha madaktari wathibitishe kuwa asingeweza kurejea katika hali yake ya kawaida, lakini alipona baada ya kutokewa na Yesu na kumponya hali iliyomfanya ampe maisha yake kuanzia siku hiyo.
 

Kuhusu elimu yake, askofu huyo anasema amesomea masuala ya Biblia jijini Nairobi nchini Kenya katika shule ya East Africa Pastorial Theological. Hata hivyo, hajaeleza kiwango chake cha elimu alichopata.
 

Baada ya kuhitimu alianza kufanya kazi ya kumtumikia Mungu ambapo alifungua kanisa katika Jiji la Mwanza, mji mdogo wa Mugumu uliopo Serengeti, Musoma na Dar es Salaam.
 

Kwa sasa anaongoza makanisa mengi ndani na nje ya Tanzania.
Gwajima ni mume wa mchungaji Grace ambaye amezaa naye watoto watatu ambao ni Ruth, Freeman na Manase.
 

Amefanikiwa kuhubiri katika nchi mbalimbali za Afrika, Marekani, Uingereza, Uswisi, Japan, Korea Kusini, Ujerumani, China na nyinginezo.
 

Askofu huyo ambaye amejipatia sifa kutokana na staili yake anayodai kwamba anafufua wafu, alitangaza kupata Shahada ya Uzamivu (Phd) kutoka Chuo Kikuu cha Omega Global nchini Afrika Kusini na sherehe yake ilifanyika Hoteli ya Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.

KAKA YAKE AJITOKEZA

Methusela Gwajima, aliyejitambulisha kuwa ni mdogo wa Askofu Gwajima amejitokeza na kusema kuwa asili yao ni Kijiji cha Koromije Kwimba, Mwanza.
Alisema kwa sasa familia ya mchungaji huyo ipo jijini Mwanza eneo la Mkolani ambako alisema yuko mama yake mzazi na baba yake yuko jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.


 Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Methusela alisema ingawa mdogo wake anaumwa, lakini anamtaka amwombe radhi Kardinali Pengo kwa njia alizozitumia kuwasilisha ujumbe wake wakati akimchafua.


MADAI YA KUTOROSHWA

Juzi, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akidai kukamata watu 15 wakitaka kumtorosha Askofu Gwajima.

 Kamanda Kova alidai watu hao walifika hospitalini saa 9:30 usiku kwa lengo hilo.
Alisema walipekuliwa na kukutwa na begi ambalo lilikuwa na bastola aina ya Berreta yenye namba CAT5802 ikiwa na risasi tatu, risasi 17 za shotgun na vitabu viwili vya hundi za benki.


 Vitu vingine ni hati ya kusafiria yenye jina la Gwajima Josephat Mathias yenye namba AB 544809, kitabu cha hundi cha Benki ya Equity pamoja na nyaraka mbalimbali za Kampuni ya Puma, chaja ya simu, tablets, suti mbili na nguo za ndani.


GWAJIMA AIBUKA

Jana, Askofu Gwajima alivunja ukimya baada ya kukanusha taarifa za yeye kudaiwa kutaka kutoroshwa na wafuasi wake 15.

 Alisema bastola iliyokutwa katika begi lililochukuliwa wodini kwake, anaimiliki kihalali kwa ajili ya kujilinda na si vinginevyo.


 Akizungumza na waandishi wa habari wodini alikolazwa, Askofu Gwajima alisema ameshangazwa na taarifa zilizoandikwa katika vyombo vya habari kwamba wafuasi wake walitaka kumtorosha.


“Juzi baada ya kupata taarifa zilizoandikwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa nimefariki dunia, maaskofu wenzangu walikuja kuniona na kunishauri niachane na taarifa hizo huenda zilikuwa na lengo maalumu.


“Baadaye nikawaambia wachungaji wangu waende nyumbani kwangu na kuchukua begi lililokuwa chumbani ambapo ndani yake palikuwa na baadhi ya nguo pamoja na bastola na nyaraka za umiliki wa silaha hiyo pamoja na vitu vingine.


“Walifikisha begi na kuliweka hapa wodini nilikolazwa, lakini walitokea watu ambao walijitambulisha kuwa ni askari na kuomba mzigo ulioingizwa ndani na hapakuwa na ushindani nikawapa,” alisema Askofu Gwajima.

AZUNGUMZIA KUZIMIA KWAKE

Akizungumzia kuzimia kwake alipokuwa akihojiwa na polisi, alisema awali alitoa taarifa kwa askari hao kwamba alikuwa anaumwa kichwa, lakini hakusikilizwa wala kupatiwa huduma yoyote.
Hata hivyo, alisema hana mgogoro wowote na Kardinali Pengo na kwamba kilichotokea alikuwa katika kazi yake ya kukemea.

TAARIFA MBILI ZA KAMANDA KOVA
Awali Kamishna Kova alisema bastola yenye namba CAT 5802 iliyokutwa kwenye begi la Askofu Gwajima haina umiliki wa mtu yeyote.
Alisema kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini kwanini Askofu Gwajima alikuwa akimiliki silaha kinyume cha sheria.


 Alisema wanasubiri atoke hospitali ili waendelee kumhoji zaidi.

 Baadaye jana jioni, Kova alituma taarifa nyingine kwa vyombo vya habari akisema uchunguzi wa kina na wa kitaalamu umethibitisha silaha hiyo inamilikiwa kihalali na Askofu Gwajima.
Alisema risasi 17 za bunduki aina ya Shotgun yenye namba 102837 zinamilikiwa kihalali.


MAASKOFU KUMWONA IGP

Katika hatua nyingine, maaskofu na wachungaji kutoka makanisa ya Kipentekoste zaidi ya 100 leo wanatarajia kwenda kumwona Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu ili kujadili suala la Askofu Gwajima.

 Akisoma tamko hilo kwa niaba ya wenzake, Askofu Damasi Mukassa kutoka Dodoma alisema wanakwenda kumwona IGP Mangu kwa ajili kuwataka watumie weledi na uadilifu kushughulikia suala hilo.

No comments:

Post a Comment