Pamoja na baadhi ya klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kutumia mamilioni ya fedha kufanya usajili wa wachezaji kwenye dirisha dogo mwezi Desemba mwaka jana, nyota wengi waliosajiliwa na timu hizo wameshindwa kuzisaidia timu zao kwa kiasi kikubwa.
Miongoni mwa timu zilizofungua pochi kwenye kipindi hicho ni Ndanda, Mbeya City, Stand United, Mtibwa Sugar pamoja na Simba ambazo zilinunua wachezaji kwa mkopo, wengine kusajiliwa kwa uhamisho wa moja kwa moja.
Simba iliwanunua Juuko Murshid, Hassan Kessy, Simon Sserunkuma na Danny Sserunkuma, imenufaika na huduma ya Kessy aliyetokea Mtibwa Sugar na Murshid aliyetokea Uganda, ambao kwa kiasi kikubwa wameibadili safu ya ulinzi ya timu hiyo ambayo inaonekana kutulia, tofauti na mwanzoni mwa ligi.
Hata hivyo, hali ni ngumu kwa Danny Sserunkuma na mwenzake Simon kwani licha ya kuja na moto, wachezaji hao wamejikuta wakikalia benchi mara kwa mara, huku taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Simba zikieleza kuwa nyota hao wa Uganda watatemwa msimu utakapomalizika kutokana na kutomridhisha kocha Goran Kopunovic.
Mbeya City, iliyomnunua beki Juma Nyosso, bado haijaonja mchango wa beki huyo kwa kiasi kikubwa kwani akiwa ameitumikia timu hiyo mechi chache, alijikuta akikumbana na rungu la kufungiwa mechi nane baada ya kujihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu.
Naye mshambuliaji Cosmas Fred aliyesajiliwa na Mbeya City kutoka Friends Rangers ameshindwa kuonyesha makali yake mpaka hivi sasa yaliyoifanya timu hiyo ya Mbeya kumwaga noti kumsajili.
Anayefunga orodha ya wachezaji waliochemsha ni kipa Alphonce Majogo aliyenunuliwa na Yanga kutoka Friends Rangers.
No comments:
Post a Comment