Tuesday, 17 March 2015

MIGIRO AWATINGIA MAASKOFU TANZANIA ... OHOOOO!! >>

migiro 

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro amewajibu maaskofu akisema Serikali haiko tayari kuona wananchi wanafundishwa jinsi ya kupiga kura kuhusu Katiba Inayopendekezwa.
Amesema ni muhimu wananchi waachwe waamue kwa utashi wao wenyewe.


Dk. Migiro amesema Serikali inaunga mkono tamko lililotolewa na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kuhusu mustakabali wa Katiba na si makundi ya watu na viongozi wa dini waanze kuingilia uamuzi wa wananchi.


Ametoa kauli hiyo siku tatu baada ya Jukwaa la Kikristo Tanzania kutoa tamko la kuwataka Wakristo wote Tanzania kujitokeza kwa wingi na kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kisha kuipinga Katiba mpya kwa kupiga kura ya hapana.


Waziri alikuwa akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, ambao walitaka kujua msimamo wa Serikali kuhusu mchakato wa Katiba Inayopendekezwa baada ya kukabidhi nakala ya Katiba hiyo kwa taasisi na wadau mbalimbali nchini.


Dk. Migiro alisema katu hakuna kiongozi mwenye mamlaka ya kumchagulia mtu namna ya kupiga kura kwa sababu kila Mtanzania ana akili timamu na ana uwezo wa kuamua kwa utashi wao.
Alisema wanapaswa kufanya uamuzi wao wenyewe bila ya kulazimishwa na kiongozi yeyote wa dini au siasa.
“Sisi tamko lile tumeliona, lakini tulishangazwa kuona viongozi wa dini wanakuwa sehemu ya kuwafundisha waumini wao jinsi ya kupiga kura katika Katiba Inayopendekezwa.
“Tumeshtushwa … tukasema kuwa wananchi ni watu makini ambao hawawezi kushawishiwa na mtu bali wanapaswa kufanya uamuzi kwa utashi wao wenyewe,” alisema Dk. Migiro.
Akizungumza huku akinukuu kauli ya Kardinali Pengo, alisema kauli ile imetolewa na kiongozi makini mwenye kupenda maendeleo kwa Taifa lake.
“Naomba nimnukuu Kardinali Pendo katika kauli yake, alisema kuwa; ‘wananchi wapewe fursa ya kufanya uamuzi wao wenyewe bila ya kushinikizwa na mtu yeyote kwa sababu hata Mungu hawezi kukuamulia baadhi ya mambo unayotaka kufanya.”
Waziri alisema kauli hiyo ya Pengo imeitia faraja serikali na kuona kuwa baadhi ya viongozi wa dini wako sambamba nayo na kwamba wana malengo ya kuhakikisha wanavuka salama katika mchakato wa kupata Katiba Mpya.
“Kwa kweli kauli ya Pengo imetutia faraja sana, tumeona kuwa kumbe kuna baadhi ya viongozi wa juu wa Kanisa wameamua kutuunga mkono katika suala hili,” alisema.


Dk. Migiro alisema Serikali ina dhamira ya kweli ya kuhakikisha mchakato huo unavuka salama wananchi waweze kupata Katiba bora ambayo itatoa mwongozo wa utendaji wa Serikali na jamii kwa ujumla.
Alisema kutokana na hali hiyo, Serikali imechapisha nakala milioni mbili ziweze kusambazwa mijini na vijijini jambo ambalo linaweza kutoa fursa kwa wananchi kuipata, kusoma na kuielewa.


Alisema kati ya hizo, nakala 1,141,300 zitagawiwa Tanzania Bara ambako kila kata itapata nakala 300.
Alisema kwa Zanzibar zimepeleka nakala 200,000 ambazo zilikabidhiwa katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ziweze kusambazwa kama ilivyokusudiwa.


Dk. Migiro alisema nakala 658,700 zimetolewa kwa ajili ya taasisi mbalimbali za serikali, asasi za raia, wizara, na makundi mbalimbali ya jamii.


Katika machapisho hayo, kuna nakala zilizoandaliwa kwa nunda nunda na maandishi makubwa ili kila mmoja aweze kupata fursa ya kuisoma na kuielewa, alisema.
Alisema mpaka sasa mchakato wa kusafirisha vitabu hivyo umekamilika ambako kila mkoa, wilaya na vijiji zimepata nakala hizo.
“Tunawaomba wananchi waisome na kueilewa waweze kufanya uamuzi wao wenyewe kwa sababu katiba hii imeandaliwa kwa lugha nyepesi ambayo inamfanya kila mmoja kuijua,”alisema Dk. Migiro.
Alisema kura ya maoni ya Katiba Mpya itafanyika kama ilivyopangwa Aprili 30 mwaka huu, ambako mchakato wa uandikishwaji wa wapiga kura unaendelea na kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
“Hatua ya uandikishwaji inaendelea kama kawaida, hakuna tatizo lolote, tunaamini NEC inaweza kufanya kazi yake kama ratiba ilivyopangwa,”alisema.
 

MTIKILA

Akizungumzia kuhusu Mwenyekiti wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila ambaye amewasilisha pingamizi, alisema Mchungaji huyo ana haki ya katiba ya kuweka pingamizi lakini wanasheria wa mahakama wataangalia sheria na kutoa uamuzi.
“Huwezi kumzuia mtu kuweka pingamizi kwa sababu ni haki yake ya katiba, ila sheria zipo na wanasheria wataangalia vipengele vya sheria waweze kutoa uamuzi kuhusu pingamizi hilo,”alisema.
 

AWAASA WAANDISHI

Dk. Migiro aliwaasa waandishi wa habari kutumia kalamu zao vizuri kuelimisha wananchi juu ya Katiba Inayopendekezwa.


Alisema bila kufanya hivyo wanaweza kuwachanganya wananchi na kushindwa kutumia haki yao ya katiba ya kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa.
“Ninawaomba waandishi wa habari mtumie kalamu zenu vizuri muweze kuelimisha wananchi juu ya Katiba Inayopendekezwa na kujitokeza kuipigia kura. Bila ya kufanya hivyo mchakato huu unaweza kukwama,”alisema.
Alisema waandishi wanapaswa kuisoma katiba hiyo waweze kuielewa na kuelimisha wananchi kwa usahihi.

No comments:

Post a Comment