Saturday, 28 March 2015
LOWASSA AWAKOROGA MA SHEIKH BAGAMOYO ..>>
EDWARD LOWASSA ..
SIKU chache baada ya Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) Wilaya ya Bagamoyo kuwakana masheikh 50 kutoka wilayani humo waliokwenda mjini Dodoma kumshawishi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kugombea urais, masheikh hao wamejitokeza na kuthibitisha kutambuliwa kwao na BAKWATA.
Msemaji Mkuu wa masheikh hao, Alhaji Hassan Kilemba jana aliitisha mkutano wa waandishi wa habari mjini Bagamoyo akielezea kusikitishwa na kauli iliyotolewa na Sheikh Mkuu wa Bagamoyo, Abdulkadir Ramiya ikikana kuwatambua.
Alisema kauli ya Sheikh Ramiya imewasikitisha kwa sababu imewavunjia heshima na kuwafanya waonekana watu wasiofaa mbele ya jamii kwa kutambulika kuwa ni Masheikh wa bandia wakati wanatambuliwa na BAKWATA.
“Sisi pamoja na kuungama wazi kuwa safari yetu haikuwa na msukumo wowote wa BAKWATA Wilaya ya Bagamoyo, ajabu Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo ambaye pia ni Sheikh wa Tarikatul Kadirya aliitambua safari yetu kwa sababu tulimpa taarifa kabla ya kuianza.
“Tumesikitishwa na kauli ya Sheikh Mkuu kuwa haitambua safari yetu ya Dodoma wakati tulimtaarifu kabla na akatukubalia…ametugeuka baada ya vigogo wa CCM kumfuata,” alisema Sheikh Kilemba.
Alisema watanzania wanapaswa waelewe vizuri kutambulika kwao na BAKWATA kwa sababu wakiwa safarini ulifanyika uchaguzi mkuu wa kuwapata viongozi wa baraza hilo wa Wilaya ya Bagamoyo na Masheikh wawili kati ya 53 waliokuwa kwenye msafara wa kwenda Dodoma walichanguliwa.
“Mimi Sheikh Kilemba binafsi sikuwapo kwenye uchaguzi huo lakini jina langu lilichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya BAKWATA wa Wilaya ya Bagamoyo,” alisema.
Naye Sheikh Sharifu Muhidin Mapanga, akizungumzia kauli ya kukanwa na kiongozi wake wa kiimani, alisema imemsikitisha kwa sababu ina lengo la kumuweka kwenye kundi la viongozi wa dini ambao ni bandia wakati ana nafasi kubwa ya zaidi ya Sheikh.
Alisema kwa kawaida Masheikh ni watu wanaopata cheo cha kidini lakini kwa upande wake anayo nafasi nyingine inayolingana na wadhfa wa uchifu.
“Hata Rais Jakaya Kikwete hawezi kuniita Sheikh bandia mimi kwa sababu anaitambua nafasi yangu katika jamii, ananitambua vizuri na nimemsaidia kama ninavyofanya leo kwa Lowassa.
“Safari yetu ya kwenda Dodoma haikuwa na ushawishi wowote wa pesa bali tulifanya hivyo kwa mapenzi ya mioyo yetu kwa sababu ya sisi kwa nafasi yetu ya kuwa viongozi wa dini tunatambua uwezo na utendaji kazi wa Lowassa. Anayekubarika na wengi ni wa Mungu kwa hiyo tumempa baraka zetu zote hivyo hata kama litatokea lolote ataendelea kuwa na baraka zetu,” alisema.
Alipotafuta Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ramiya kupitia simu yake ya kiganjani ili atoe ufafanuzi wa kauli yake dhidi ya shutuma alizoelekezewa na viongozi wenzake za kuwashushia hadhi mbele ya jamii iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu yake haikujibiwa.
Machi 21 mwaka huu, Masheikh zaidi ya 50 wa Bagamoyo walikwenda nyumbani kwa Waziri Mkuu wa zamani, Lowassa mjini Dodoma kwa nia ya kumshawishi agombee urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Ushawishi wa masheikh hao kwa mara ya kwanza ukamfanya azungumzie suala hilo kwa kueleza kuwa ameshawishika kuchukuwa fomu ya kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) muda utakapofika na kwa kufuata taratibu zilizowekwa na chama chake.
Akizungumza na Masheikh hao ambao pia walimchangia sh 700,000 kwa ajili ya kwenda kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na CCM kuwa mgombea wake, alisema kwa muda mrefu amekuwa akipata ushawishi kutoka makundi mbalimbali ya jamii lakini ushawishi wa viongozi hao wa dini ulikuwa na uzito wa kipekee.
Siku moja baada ya Masheikh hao kufika nyumbani kwa Lowassa, uongozi wa BAKWATA Wilaya ya Bagamoyo uliwakana kwa kile ulichoeleza kuwa haukuwatuma kwenda Dodoma kumshawishi Lowassa agombee urais wala haukuhusika kumchangia fedha za kwenda kuchukulia fomu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment