Saturday, 28 March 2015

GWAJIMA AJISALIMISHA POLISI .. ATAKIWA KWA DC ... >>

 

Wakati  Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima akijisalimisha kwa Jeshi la Polisi, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda amemtaka aripoti ofisini kwake keshokutwa kutoa maelezo kuhusiana na tuhuma za kumkashifu kiongozi mwenzake wa dini. 
                              
Juzi, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ilitoa amri kwa askofu huyo kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kutoa maelezo kuhusu tuhuma za kashfa na matusi dhidi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Askofu Gwajima alitii amri hiyo na jana alifika kituoni hapo saa 8.15 mchana kwa ajili ya kutoa maelezo.

Akizungumza muda mfupi kabla ya kwenda kutoa maelezo, Askofu Gwajima alisema Baraza la Maaskofu Tanzania, lilikubaliana kupinga Mahakama ya Kadhi lakini Askofu Pengo akawageuka..

“Tulikubaliana kwa pamoja kwamba hatutaki na viongozi wote tulisaini makubaliano hayo akiwamo Kardinali Pengo lakini tunashangaa alitugeuka,” alisema na kuongeza:

“Mimi kama kiongozi wa kiroho nilimkemea kiongozi mwenzangu wa kiroho.”

Alisema katika maneno aliyotoa hakuna neno lolote ambalo ni la kashfa...“yale yote ambayo nimeongea ni maneno kutoka kwenye Biblia. Kwa hiyo leo (jana) nimeshangaa kuitwa na polisi. Nilitarajia kama kuitwa angeitwa yeye (Kardinali Pengo),” alisema Askofu Gwajima na kuongeza kuwa, aliitikia wito huo ili kufahamu ni kwa nini ameitwa. Mapema wiki hii, mitandao mbalimbali ya kijamii, ilisambaza sauti ya Askofu Gwajima akitoa maneno makali ya kumkashifu Kardinali Pengo.

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema: “Taratibu za mahojiano zimeanza kwa mujibu wa sheria na mtuhumiwa  atapewa haki zote anazostahili kama vile kuwa na ndugu na rafiki yake wa karibu anayemwamini au wakili wake.”

Akizungumzia kuhusiana na tuhuma zinazomkabili Askofu Gwajima, Kova alisema ni pamoja na kumkashifu na kumtukana hadharani Kardinali Pengo.

Kuitwa kwa DC Kinondoni

Katika hatua nyingine, Makonda amemwandikia barua Askofu Gwajima akimtaka kufikia ofisini kwake kutoa ufafanuzi juu ya maneno makali dhidi ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki.

Katika barua yake, Makonda alisema ofisi yake inataka kufahamu kama uhuru wa kuabudu kikatiba ni kutokuheshimu watu wengine. “Hatuamini kama imefika wakati kwenye nyumba za ibada kumegeuka sehemu ya kutukana na kuwasema watu badala ya kuhubiri habari njema. Tunataka kujidhihirisha malengo hasa ya kutumia maneno hayo ni nini.”

No comments:

Post a Comment