Tuesday, 17 March 2015

KUELEKEA UCHAGUZI MKUU TAIFA NJIA PANDA ...>>

  

Wakati Taifa likijiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, yamebainika mambo matatu mazito ambayo yanaliweka njiapanda , hali inayosababisha viongozi na hata wananchi kubaki na maswali lukuki wakihoji hatma ya nchi yao.

Mambo hayo ambayo hadi sasa hayajulikani hatma yake ni Katiba Inayopendekezwa, Mahakama ya Kadhi na uboreshaji wa Daftari la Wapigakura kwa vifaa vya kielektroniki vya Biometric Voter Registration (BVR).
Mambo hayo yamekuwa  mjadala wa kitaifa kwa muda sasa, hoja kubwa ikiwa ni endapo matukio makubwa ya kitaifa – upigaji wa kura ya maoni kupitisha Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba yatafanyika kwa mafanikio au yanaweza kukwama na kusababisha sintofahamu.

Uandikishaji BVR
Hoja kubwa katika eneo hili imekuwa ni iwapo kura ya maoni ya kupitisha Katiba itafanyika Aprili 30, mwaka huu kama ilivyopangwa, lakini Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva mara kadhaa amesimamia msimamo wa Serikali kuwa uandikishaji unaendelea bila matatizo katika Mkoa wa Njombe kama ilivyopangwa.
Ukiacha upungufu unaosababisha shughuli hiyo kuchukua muda mrefu, Jaji Lubuva amekuwa akikwepa kuzungumzia madai kuwa Serikali haikutoa fedha za kutosha kufanikisha shughuli hiyo, lakini juzi alikiri kuwa Tume yake ilijaribu hata kuazima vifaa hivyo Kenya na Nigeria bila mafanikio.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amekaririwa na gazeti hili jana akisema hata bajeti ya mchakato huo ya Sh297 bilioni  iliyopangwa haipo kwa kuwa katika kasma ya tume zilikutwa Sh7.01 bilioni na fedha za maendeleo na fedha za tume hazikuonekana.
Profesa Lipumba alisema pia hata Sh144 bilioni za kura ya maoni zilizoelezwa na Tume hazikuonekana kwenye vitabu vya bajeti na kuwa BVR 250 zilizopo badala ya 8,000 zilizokusudiwa haziwezi kufua dafu.
Kuhusu muda uliosalia wa siku 42 kabla ya kura ya maoni, umeelezwa na wachambuzi kuwa hautoishi, ukilinganishwa na Kenya iliyokuwa na BVR 15,000 na ikaandikisha wapiga kura milioni 14 kwa siku kati ya 45 hadi 60.
Kutokana na hali hiyo, kinachosubiriwa na wananchi ni ama kuelezwa ni muujiza gani utafanyika hadi shughuli hiyo kukamilika na kura ya maoni kupigwa bila matatizo au kuahirisha kura hiyo hadi wakati au baada ya uchaguzi mkuu.
Mahakama ya Kadhi       
Saula jipya kabisa katika mjadala wa uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi inayotambuliwa na Serikali ni kesi iliyofunguliwa Mahakama Kuu na Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila akitaka mahakama itamke kuwa Mahakama ya Kadhi na masuala ya Jumuiya ya Kiislamu (OIC) ni haramu na itamke kuwa ulinzi na uhai na utu wa binadamu nchini hauwezi kubaguliwa na Uislamu.

No comments:

Post a Comment