Tuesday, 31 March 2015

KIMENUKA JUZI ZNZ .. KINOOOOMA .. NI SHEEEDAH SIASA ZNZ ..! >>




TUTOKE VIPI ?



1234                                                                   Zanzibar

HALI ya usalama visiwani Zanzibar imechafuka baada ya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), kuvamiwa na kupigwa na watu wanaodaiwa kuwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kutokana na vurugu hizo, watu 25 waliokuwa wakitokea katika mkutano wa CUF uliokuwa unafanyika Makunduchi, Wilaya ya Kusini Unguja wamejeruhiwa, huku wanne kati yao wakilazimika kuhamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Saadi Juma Khamis, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 1:30 usiku katika maeneo ya Fuoni ambapo watu waliokuwa wamejificha pembeni mwa barabara walianza kuwashambulia wafuasi hao wa CUF waliokuwa katika gari mbili aina ya Fuso zenye namba za usajili Z 279 EH na Z 678 GB.


 Kamanda Saadi alisema kwa mujibu wa taarifa za awali za jeshi hilo, wahalifu hao baada ya kufanya shambulizi la kushtukiza walitokomea kusikojulikana ambapo majeruhi walipelekwa katika Kituo cha Polisi Mwanakwerekwe kupewa fomu namba tatu kwa ajili ya matibabu.
“Majeruhi wa tukio hili wameumia katika sehemu mbalimbali za miili yao ikiwamo kuvunjika taya, mikono na hata kutobolewa macho.
“Watu wote waliopatwa na mkasa huu wapo katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa matibabu zaidi,” alisema Kamanda Saadi.
Alisema baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa za tukio hilo, wameanza upelelezi ili kuweza kuwabaini wahalifu wa tukio hilo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.


 Kamanda Saadi aliwataja majeruhi kuwa ni Omar Salum, Khamis Juma Khamis, Khatib Khamis, Salum Abdalla Mtumwa, Mariam Juma Mohamed, Ali Shaame Mohamed, Hemed Salum Hemed, Khan Khali Gharib, Hamad Ali Hamad na Abdillah Abas Khamis.

 Wengine ni Mohamed Salum Mbarouk, Said Hamad Hassan, Makame Nassour na Masoud Mohamed Tahir ambao wote ni wafuasi wa CUF Zanzibar.

MAALIM SEIF: HATUJIBU MAPIGO

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema pamoja na wanachama wake kufanyiwa unyama huo, katu chama chake hakitajibu mapigo dhidi ya watu hao.
Alisema badala yake wanaendelea kufanya siasa za kistaarabu kwa kujenga hoja.
Maalim Seif alitoa kauli hiyo jana mjini Unguja baada ya kuwajulia hali majeruhi wa tukio hilo ambapo aliituhumu CCM kuhusika na mkakati huo kwa kupandikiza chuki kwa vijana ili waweze kufanya uhalifu huo.
“Hivi sasa CCM haifanyi siasa za kistaarabu bali wameamua kufanya hujuma na ukatili wa kupindukia juu ya CUF jambo ambalo si malengo ya kuanzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
“CUF hatuchokozeki japo wenzetu wanaandaa mbinu mbalimbali ili tuweze kuingia katika vurugu na tunachowambia ni kwamba haya yote wanayoyafanya mwisho wake ni mwaka huu,” alisema,
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, alisema CUF haitojibu mashambulizi ya aina yoyote, ila kwa sasa wanajipanga kuindoa CCM madarakani Oktoba mwaka huu.


“Natumia fursa hii kuwataka vijana wetu wa CUF wasifanye vurugu wala kulipiza kisasi, bali waendelee kushikamana na kuheshimu sheria huku wakijipanga kuiweka CUF serikalini mwaka huu,” alisema Maalim Seif.

 Mmoja wa majeruhi, Ali Shaame Mohamed (28), alisimulia tukio hilo na kusema baada ya kufika katika eneo la Fuoni waliona gari aina ya Fusso likitokea pembeni yao na kuanza kurushiwa unga uliokuwa na chupa zilizosagwa.

 Alisema watu waliokuwa katika gari hilo wakiwa na mapanga, marungu, chupa, nondo na mawe ambao walianza kuwapiga.
“Wale vijana baada ya kushuka katika gari lao walituzingira na kuanza kutupiga kwa mapanga na marungu, lakini hata leo hii kuwa hai ni kwa mapenzi ya Mungu,” alisema Ali.
Awali katika mkutano uliofanyika juzi Makunduchi, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alitoa taarifa jukwaani kwa kulitaka Jeshi la Polisi kuwadhibiti vijana waliokuwa wameandaliwa kufanya tukio hilo.

No comments:

Post a Comment