Taarifa kutoka Somalia zinasema
kundi la kigaidi la Al Shabaab limeuchukua mwili wa kiongozi wao
anayedaiwa kuuwawa na kombora la Marekani.
Adan Garar ameripotiwa kuuwawa akiwa ndani ya gari siku ya alhamisi, kwenye shambulio hilo lililotekelezwa na Marekani.
Watu wengine wawili waliokuwa wakisafiri naye pia wameuawa.
Garar alishukiwa kuandaa shambulizi la kigaidi kwenye jumba la Westgate mnamo mwaka wa 2013, ambapo watu sitini na saba waliangamia.
Aidha taarifa zingine zinasema Garar alikuwa akipanga mashambulio sambamba katika mji wa Mombasa pwani ya Kenya, ambapo Polisi wa kupambana na ugaidi walinasa gari moja ambalo lilikuwa limejaa vilipuzi, ambavyo, wanasema vilikuwa vikilengwa kwenye maeneo ya watu wengi.
Kundi la Al shabaab limekuwa likitekeleza mashambulio ya kigaidi ndani ya Kenya kutokana na wanachokitaja kama kulipiza kisasi dhidi ya mashambulio ya vikosi ya Kenya chini ya mwamvuli wa Amisom, kikosi cha Umoja wa Afrika kinacholinda amani Somalia.
Marekani imetumia makombora mara kadhaa kuwalenga makamanda wa Al Shabaab ndani ya Somalia.
Ni katika shambulio kama hili ambapo aliyekuwa kiongozi mkuu wa AL Shabaab, Ali Godane aliuwawa Septemba mwaka uliopita .
Vilevile kumekuwa na mashambulio mengine mengi ambayo yamedaiwa kulenga kambi za kundi hilo, bila thibitisho lolote.
No comments:
Post a Comment