Jana ilikuwa siku ya hisia tofauti kwa watu wawili wanaotajwa kwenye kinyang’anyiro cha urais, Edward Lowassa na Lazaro Nyalandu baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kumsifu mmojawao na kumponda mwingine.
Akiwa Kondoa, Kinana alitumia muda mwingi kujibu
kilio cha wananchi wanaosumbuliwa na askari wa wanyamapori kwa kumponda
Waziri Nyalandu kuwa anazurura bila kushughulikia matatizo ya wananchi,
lakini saa chache baada ya kuwasili Monduli alimsifu Lowassa kuwa ni
kiongozi shupavu.
Tayari Nyalandu ameshatangaza nia ya kugombea
urais, wakati Lowassa, mmoja wa wanachama wa CCM wanaotajwa sana kwenye
kinyang’anyiro hicho, hajatangaza uamuzi wake lakini anatumikia adhabu
ya chama chake kilichomfungia kujihusisha na harakati za uongozi pamoja
na makada wengine watano.
Baada ya msafara wa Kinana kuwasili Monduli na
kupokewa na viongozi wa chama hicho wa eneo, katibu huyo wa CCM, Kinana
alipata nafasi ya kuzungumza machache kabla ya kuanza safari ya kukagua
shughuli mbalimbali.
“Hatuna shaka na Monduli kwa kuwa yupo kiongozi
shupavu, ndugu yetu Waziri Mkuu mstaafu na mjumbe wa (Halmashauri Kuu ya
CCM) Nec,” alisema Kinana akiwaelezea wananchi waliokuwapo eneo hilo.
“Wa Monduli mna kiongozi shupavu na mchapakazi. Hongera Bwana Lowassa.”
Baadaye, Lowassa aliwakaribisha akisema: “Mmefanya kazi kubwa sana ya kukijenga chama chetu. Nawashukuru sana, karibuni.”
Naye katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nnauye alisema: “Nafurahi kuwa katika jimbo la mzee wangu, rafiki yangu
Edward Lowassa. Mapokezi mazuri, bila shaka Arusha mmeamka.”
Kinana amekuwa akitumia sehemu kubwa ya ziara yake
kushuhutumu viongozi wa Serikali na hasa mawaziri kwa kushindwa
kuwatatulia wananchi matatizo yao na ilifikia wakati aliwataja mawaziri
wanne aliowaita kuwa ni mizigo, tofauti na alivyofanya kwa waziri mkuu
huyo wa zamani.
Lowassa alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Serikali
ya Awamu ya Nne na anajulikana kama mtu aliye tayari kufanya uamuzi
mgumu. Alilazimika kujiuzulu wadhifa huo mwaka 2008 baada ya kuibuka kwa
kashfa ya Richmond.
Kinana alikuwa mtu tofauti wakati akijibu kero za
wananchi mkoani Singida, ambako alimtaja moja kwa moja Waziri Nyalandu
kuwa hashughulikii matatizo ya wananchi na badala yake amekuwa
akizunguka bila msaada wowote.
Kinana alisema hayo juzi katika Kijiji cha
Ikengwa, Kata ya Kinyasi wilayani Kondoa baada ya wananchi wa kijiji
hicho kumchongea Nyalandu kwa Kinana kwamba wizara yake inawaua na
kuwaumiza bila ya hatia, hivyo wamechoka.
No comments:
Post a Comment