Sunday, 15 March 2015
SAKATA LA KUMUUA DR. SLAA LAONGEZAA WADAU .. WANACHAMA WATATU WAFIKISHWA KIZIMBANI .. >>
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limeanza kumchunguza Josephine Mushumbusi, ambaye ni mke wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, anayetuhumiwa kula njama za kumuangamiza.
Uchunguzi dhidi ya Mushumbusi ulitangazwa jana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyia ofisini kwake, Dar es Salaam.
Kamishna Kova alisema kuanzishwa kwa uchunguzi huo ni matokeo ya maelezo ya Khalidi Kangezi, ambaye alikuwa mlinzi wa Dk. Slaa aliyefikishwa polisi baada ya kuteswa na kutekwa kwa tuhuma za kushiriki mipango ya kumuua bosi wake huyo.
Alisema, Kangezi baada ya kufikishwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, katika maelezo yake aliwataja Mushumbuzi na mchungaji mmoja ambaye jina lake halijawekwa hadharani kuwa ndio waliokuwa na mpango huo, lakini yeye aliuzuia
Mbali na wawili hao, Kamanda Kova alisema uchunguzi huo pia utawagusa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula, ambaye ametajwa na baadhi ya makada wa chama hicho kuwa mmoja wa wahusika wa mpango wa mauaji ya Dk. Slaa.
Wakati Jeshi la Polisi likitangaza kuanzishwa uchunguzi huo, wanachama
watatu wa Chadema wanaotuhumiwa kumteka na kumtesa Kangezi, jana walishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kutenda makosa mawili.
Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali, Janeth Kitali, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Warialwande Lema, majira ya saa nane mchana.
Wakili Kitali alidai mahakamani hapo kuwa kosa la kwanza la washtakiwa, Diwani Boniface Jacob (32), Mlinzi Hemedi Sabula (48) na Ofisa Utawala wa chama hicho, Benson Mramba, ni kumjeruhi Kangezi, kosa ambalo walilitenda Machi 7, mwaka huu.
Katika shtaka hilo washtakiwa wanadaiwa kwamba tarehe hiyo wakiwa Makao Makuu ya Ofisi za Chadema zilizopo Mtaa wa Ufipa, Kinondoni Dar es Salaam, walimjeruhi Kangezi kwa kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia maumivu makali.
Aliendelea kudai kuwa tarehe na eneo walipofanya kosa la kwanza, walitenda kosa jingine la kumteka Kagenzi na kumpeleka katika Hotel ya River View Hotel iliyopo Sinza, Kinondoni, Dar es Salaam, kwa nia ya kumnyima uhuru wake
Washtakiwa hao wanaotetewa na Wakili Peter Kibatala na John Malya, walikana mashtaka yote na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo kesi iliahirishwa hadi Machi 26 mwaka huu, itakapotajwa tena.
Hakimu Lema aliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja ambao wanatoka katika taasisi inayotambulika au serikalini isipokuwa walimu. Wadhamini hao walipaswa kusaini hati ya dhamana ya maandishi ya Sh milioni 10.
Washtakiwa walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kupelekwa gereza la Keko hadi hapo upande wa mashtaka utakapomaliza kufanya ukaguzi wa barua za wadhamini wao kuona kama wamekidhi vigezo.
Kabla ya kupandishwa kizimbani kwa washtakiwa hao, Kamishna Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa kitendo cha makada watano wa Chadema cha kumuweka chini ya ulinzi na kumtesa kwa muda wa saa 15 Kangezi ni kosa kisheria, hivyo Jeshi la Polisi limewafunguliwa shauri la kushambulia hadi kumjeruhi mlinzi huyo.
Kova alisema Jeshi la Polisi limechukua uamuzi huo kutokana na maelezo pamoja na majeraha aliyoyapata Kangezi mara baada ya kufikishwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay.
Alisema, ingawa Wakili wa Chadema, John Malya alimfikisha Kangezi katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay na kumfungulia shitaka la kupanga njama za kumuangamiza Dk. Slaa kwa kumuwekea sumu kwenye maji au chakula, Kangezi kwa upande wake alitoa maelezo ya kutekwa nyara na makada watano wa Chadema ambao walimuweka chini ya ulinzi na kumtesa hadi kumuumiza.
“Tumefungua mashauri mawili, la kwanza ni uchunguzi dhidi ya tuhuma na mpango wa kutaka kumdhuru Dk. Slaa na pili ni uchunguzi dhidi ya watuhumiwa wanaodaiwa kumtesa kwa kumshambulia Kangezi na kumsababishia majeraha mwilini mwake,” alisema Kamishna Kova.
Kamishna Kova alisema kutokana na maelezo ya Kangezi, Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watuhumiwa waliotajwa na Kangezi kuhusika kumtesa na kumteka.
Alisema baada ya uchunguzi wa awali wa mashauri yote mawili kukamilika, yatapelekwa kwa Wakili wa Serikali ili wote wanaohusika katika suala hilo wafikishwe mbele ya sheria.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment