Serikali inakusudia kuwasilisha bungeni, miswada miwili ya Haki
ya Kupata Habari na ule wa Huduma za Vyombo vya Habari ili iweze
kupitishwa kuwa sheria.
Wadau wa habari, ambao wamekuwa wakipigania kupata
sheria itakayowapa uhuru wa kukusanya, kuandika na kusambaza habari kwa
kuzingatia maslahi ya taifa, watafurahi kuona rais wao anasaini, kuwa
sheria, miswada yenye maudhui rafiki, lakini si kama ilivyo kwa miswada
hii miwili.
Harakati za wadau wa habari zilianza katikati ya
miaka ya 1990, kupigania chombo huru cha kusimamia wanahabari ambacho ni
Baraza la Habari Tanzania (MCT) na itungwe sheria mpya itakayotoa uhuru
wa habari.
Baadaye walijikusanya na kuandaa miswada miwili;
mmoja ni wa Haki ya Kupata Habari na wa pili ni wa Huduma za Vyombo vya
Habari na wakawasilisha serikalini. Serikali ilipokea miswada hiyo na
iliahidi kuiwasilisha bungeni, kwa mara ya kwanza mwaka 2007.
Hata hivyo, haikuwasilisha miswada hiyo, badala
yake ilianza kuhangaika kutunga vipengele vya marekebisho ya sheria ya
magazeti ya mwaka 1976 na sheria ya utangazaji ya mwaka 1993 kuongeza
vifungo, faini ya mamilioni ya shilingi na kesi zilizofunguliwa dhidi ya
mwanahabari aliyeshitakiwa kwa kuandika habari za kashfa ziharakishwe
kusikilizwa. Wabunge walikataa marekebisho hayo wakataka Serikali
iwasilishe sheria nzima kama ilivyokubaliwa na wadau wa habari.
Katika namna inayoshangaza, baada ya danadana za
muda mrefu, Serikali iliwasilisha miswada hiyo katika Bunge la Februari
ijadiliwe, chini ya hati ya dharura. Wadau wa habari walijiuliza, kwa
nini Serikali iwasilishe miswada hiyo kwa dharura? Kwa nini iwasilishe
miswada hiyo bila kuwapa wadau fursa ya kujadili maudhui yake? Je,
Serikali inaogopa nini kukutana na wadau wa habari kujadili miswada
hiyo?
Kumbe Serikali iliingiza vipengele ambavyo si
rafiki kwa wadau wa habari kwani badala ya kukuza uhuru na maadili ya
habari vinakandamiza uhuru na kupora haki yao kama ilivyoainishwa katika
Ibara ya 18 ya Katiba.
Katika miswada hiyo, imependekezwa: Kiwango cha
elimu kwa mwanahabari kiwe shahada ya kwanza; mtu haruhusiwi kumiliki
vyombo vingi vya habari; mwandishi atakayepatikana na kosa faini Sh20
milioni au kifungo kisichopungua miaka mitano au adhabu zote mbili kwa
pamoja kwa mshitakiwa atakayethibitishwa na mahakama kutenda kosa.
Vilevile, imependekezwa vyombo vya habari vya
binafsi kutakiwa kujiunga na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) saa
2.00 usiku kila siku kwa ajili ya taarifa ya habari. Vipengele hivi ni
vizito na havifai.
Ni jambo zuri kwa mwanahabari kuwa na elimu nzuri
ili aweze kuwa na umilisi wa kazi yake ya kuhabarisha na kuelimisha
jamii, lakini tunajiuliza kwa nini sharti la elimu ya juu liwe kwa
wanahabari tu na siyo kwa walimu, mahakimu, na viongozi? Kwa nini
Serikali inatunga sheria kuvibana vyombo vya habari vya hapa nchini na
siyo vya kimataifa?
Kwa nini mkazo wa adhabu usiwe kwa mafisadi,
wabadhirifu wa mali ya umma badala yake Serikali imewalenga wanahabari?
Kwa nini Serikali imevizia dakika za mwisho na kuanzisha mgogoro na
wadau wa habari tena kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu?
Tunawaomba wabunge, wapitie miswada hiyo kwa
umakini, waisome na kukataa vipengele vyote ambavyo havitoi afya njema
kwa tasnia ya habari. Wanahabari wanahitaji uhuru na jamii inataka uhuru
kwa kusoma na kusikia habari wanazotaka kutoka vyombo binafsi bila
kulazimishwa kwa sheria.