Monday, 25 May 2015

Baada ya mauaji ya kiongozi wa upinzani Zedi Feruzi Jumamosi Jioni, vyama vya siasa na mashirika ya kiraia yanayopinga muhula wa tatu wa rais Pierre Nkurunziza yamechukua uamzi wa kusitisha mazungumzo na serikali, na kutoa wito kwa wafuasi wao kuanzisha maandamano tangu leo Jumatatu.

Hata hivyo, Umoja wa Mataifa umehakikisha kwamba mazungumzo yataendelea, suala la muhula wa tatu wa rais Nkurunziza kwa sasa halitakiwi kuwekwa mezani, kwani rais huyo hana haki ya kuwania muhula wa tatu, amesema kiongozi wa shirika linalopiga vita ufisadi wa mali ya umma Olucome, Gabriel Rufyiri, mmoja kati ya wanaharakati wanaopinga muhula wa tatu wa rais Nkurunziza.

Wajumbe wa vyama vya siasa vya upinzani wamesusia kikao cha mazungumzo cha Jumapili Mei 24 kiliyofanyika kwenye makao makuu ya Tume ya uchaguzi ya Umoja wa Mataifa nchini Burundi (Minub). Mazungumzo ambayo yanafanyika kwa wiki tatu sasa.

Hata hivyo wawakilishi wa mashirika ya kiraia wanaopinga muhula wa tatu wa rais Nkurunziza wameshiriki kikao hicho cha mazungumzo. Lakini Jumapili jioni wameapa kutorodi kushiriki mazungumzo hayo, na hivyo kususia wito uliyotolewa na Makanisa Katoliki na Protestanti wa kuongeza siku moja kwa muda wa siku mbili wa usitishwaji wa maandamano uliyotangazwa na mashirika ya kiraia na upinzani, muda ambao ulimalizika Jumapili jioni Mei 24.

Wajumbe wa vyama vya kiraia wametoa masharti ili waweze kurejea kwenye meza ya mazungumzo ikilinganishwa na hali ya usalama inayojiri wakati huu.
" Kwanza, tunaomba kuwepo na uchunguzi wa kina uliyo halali kuhusu mauaji ya Zedi Feruzi, na waliohusika na mauaji hayo. Kwa njia hiyo, [viongozi] wengine wanaweza kuwa na imani na usalama wao, kwa sababu wakati huu hatuna usalama wowote ", amesema Gabriel Rufyiri, mwanaharakati wa vyama vya kiraia.

Watu zaidi ya ishirini wameuawa tangu maandamano ya kupinga muhula wa tatu wa rais Nkurunziza yaanze wiki nne zilizopita.

No comments:

Post a Comment