Klabu kongwe nchini za Yanga na Simba wanaanza kupigana vikumbo kuwania saini za wachezaji waliong’ara kwenye msimu wa Ligi Kuu uliomalizika karibuni.
Wakati kocha wa Yanga Hans van de Pluijm akielezwa kuacha majina ya nyota anaowataka huku mwenyewe akielekea Ghana kwa mapumziko, Simba wameshaanza kazi.
Inaelezwa kwamba Wekundu wa Msimbazi wanasaka saini za washambuliaji Rashid Mandawa wa Kagera Sugar na Malimi Busungu wa Mgambo JKT.
Wachezaji hao ni wazuri lakini imeshangaza kwamba hawakuitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kinachoshiriki michuano ya Cosafa nchini Afrika Kusini. Inadaiwa kwamba bado Simba wapo kwenye mazungumzo na wachezaji hao.
Pamekuwapo na mgawanyiko miongoni mwa vigogo wa Simba juu ya kumrejesha kipa wao wa zamani, Juma Kaseja anayesugua benchi Yanga na ambaye ameshitakiwa na mabingwa hao wapya wa nchi.
Yanga kwa upande wao wanaelekea kupitisha fagio la chuma kuondoa wachezaji ambao kocha hawataki na kuimarisha safu ya ulinzi.
Mmoja wa wachezaji wanaowaniwa ni mlinzi wa kati, Salim Mbonde aliyewika akiwa na Mtibwa Sugar na mwingine ni beki wa Polisi Rwanda, Ngirinshuti Mwemere watakaocheza vyema na akina Mbuyu Twite.
Yanga wanahitaji kikosi imara cha wachezaji wenye utimamu wa mwili, kiwango cha juu na nguvu kwani wanashiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika msimu huu na Kombe la Kagame.
Hata hivyo, wamekuwa na tabia ya ama kujitoa Kagame au kupeleka timu ya vijana. Wamedaiwa kutishia kutocheza iwapo Simba watapewa pia nafasi humo.
Yanga wanamuwinda Said Ndemla wa Yanga lakini Simba chini ya Zacharia Hanspoppe na kasim Dewji wanadaiwa wameshamsainisha, kwani alikuwa tegemeo lao kubwa msimu uliopita.
Miongoni mwa wachezaji wanaodaiwa wataachwa na Yanga ni Danny Mrwanda ambaye licha ya umri kumtupa mkono hakuwa na msimu mzuri. Alipata kuchezea Simba kabla ya kuachwa.
Said Bahanuzi anatarajiwa kurejeshwa Yanga na Pluijm amesema atamwandaa vyema kuwa mshambuliaji hatari. Alikuwa kwa mkopo Polisi Morogoro.
Simba walioshindwana na kocha wao Goran Kapunovic anayetaka mshahara mkubwa na marupurupu mengi, wamewaondoa kikosini wachezaji wa kigeni Joseph Owino, na ndugu wawili Simon Sserunkuma na Dan Sserunkuma.
Simba wanaendelea kusajili wakiwa hawana kocha ambaye anatafutwa kutoka Ulaya Mashariki, wakisema hawana mpango na makocha wazawa
No comments:
Post a Comment