Monday, 18 May 2015

MAANDAMANO MAKUBWA BURUNDI LEO ...>>> source MTANZANIA gazeti

WAPINZANI wanaompinga Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, wametangaza kufanya maandamano makubwa ya kupinga hatua ya kiongozi huyo kuwania urais kwa muhula wa tatu.
Pamoja na hali hiyo, Rais Nkurunziza, jana alijitokeza kwa mara ya kwanza tangu jaribio la kumpindua lishindwe na kueleza tishio la nchi yake kushambuliwa na kikundi cha wanamgambo wa Kiislamu wa Al Shabaab cha Somalia.

 Wakati akiyasema hayo, Rais Nkurunziza hakutoa kauli yoyote kuhusiana na jaribio la mapinduzi dhidi ya Serikali yake.

 Nkurunziza alijitokeza ikulu Bujumbura jana mbele ya wanahabari ambako alisema hivi sasa nchi yake inakabiliwa na tishio la ugaidi kutoka kwa kikundi cha Al Shabaab.
“Nimekuja ofisni na kuzungumza kwa simu na viongozi wa Uganda na Kenya kuhusiana na tishio la ugaidi kutoka kwa kikundi cha wanamgambo wa Kiislam cha Al shabaab,” alisema Nkurunziza.
Juzi, watu 18 walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kusaidia kufanya mapinduzi.

 Hadi sasa kiongozi wa mapinduzi hayo, Meja Jenerali Godefroid Niyombare bado yuko mafichoni huku wanaharakati wakiwa wamepanga maandamano zaidi leo kupinga uamuzi wa Nkurunziza kugombea kwa muhula wa tatu.

Mwanahabari kutoka Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Karen Allen alisema wanajeshi walioshiriki katika mapinduzi hayo walichukuliwa na polisi na kupakizwa katika gari na hadi sasa haijulikani walipo.

Allen ambaye yupo Bujumbura, alisema madai ya Rais Nkurunziza kuhusu mashambulio ya Al Shaabab huenda ikawa ni kisingizio cha kudhibiti hali ya usalama na maandamano yanayotarajiwa kufanyika leo.

Hata hivyo kuna taarifa kuwa wanajeshi wa Serikali walishambulia hospitali iliyokuwa ikiwapatia matibabu askari walioshiriki katika mapinduzi.

Rais Nkurunzinza alikuwa Dar es Salaam wakati jaribio la mapinduzi likifanyika nchini mwake. Alirejea Ijumaa iliyopita baada ya wanajeshi wanaomtii kudhibiti mapinduzi hayo.

 Maofisa wa mambo ya nje wa Uingereza na Marekani walisema Al shabaab wamekuwa wakitishia kuishambulia Burundi kwa kuwa askari wako wamo katika jeshi la Umoja wa Afrika (AU) linalolinda usalama Somalia.

 Ubalozi wa Marekani umewashauri raia wake kuondoka Burundi kwa sababu ya kuzorota kwa hali ya usalama na siasa pamoja na kuwapo tishio la Al Shabaab

CNDD NA KAMPENI

 Wakati huohuo, Chama tawala nchini Burundi cha CNDD-FDD, kimesema hakioni sababu ya kuahirishwa uchaguzi nchini humo.

 Akizungumza na MTANZANIA mjini Bujumbura jana, Msemaji wa CNDD-FDD, Ndabirabe Gelose, alisema pamoja na kutolewa ushauri na wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), uchaguzi hautaahirishwa.

 Katika mkutano wao, wakuu wa EAC, chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete waliokutana Dar es Salaam wiki iliyopita, walitoa azimio la kutaka Burundi iahirishe uchaguzi wake hadi hali ya amani itakaporejea.

 Gelose alisema wao wanaendelea kampeni za uchaguzi na wanatarajia kuufanya kama ilivyopagwa na tume huru ya taifa ya uchaguzi ya Burundi.
“Sisi tunaendelea na kampeni zetu na leo ni siku ya sita na hali ya amani inaanza kurejea hasa katika mji wa Bujumbura, ingawa kuna maeneo bado hali si nzuri.
“Ushauri wa wakuu wa EAC tumeusikia lakini kwetu sisi tunasema siyo wazungumzaji wa jambo hilo, ila tume huru ya taifa ya uchaguzi ndiyo inaweza kutoa kauli kama uchaguzi utaendelea ama laa.
“Ila sisi CNDD-FDD tunaendelea kuomba kura na sasa nazungumza na wewe si unasikia muziki, ndiyo tupo na harakati za kuomba kura kwa Warundi,” alisema Gelose
Alipoulizwa kuhusu alipo kiongozi aliyetangaza mapinduzi yaliyoshindwa, Meja Jenerali Godefroid Niyombare, alisema kwa sasa hawezi kusema yupo wapi ingawa bado anatafutwa na vikosi vya Serikali.
“Alipo Niyombare sijui ila kuna taarifa ametoroka na vikosi vya Serikali vinaendelea kumsaka,” alisema.

Kwa miezi kadhaa sasa muungano wa vyama vya upinzani ADC-Ikibri na baadhi ya mashirika ya raia wamekwisha kuondoa wajumbe wao katika tume hiyo.
Tume huru ya taifa ya uchaguzi ya Burundi (Ceni0, imekua ikinyooshewa kidole na vyama vya upinzani, mashirika ya raia na vyama vinavyounga mkono utawala wa chama tawala CNDD-FDD kwa kuchukua uamuzi bila kuwashirikisha wadau wote katika suala la uchaguzi.

TUME LALAMIKIWA

Tume hiyo imekuwa ikipingwa na vyama vya upinzani tangu ilipoteuliwa na kupitishwa na Bunge mwanzoni mwa mwaka 2014.

Hata hivyo tume hiyo ilituhumiwa katika uchaguzi wa mwaka 2010 kwamba ilipanga njama na chama tawala CNDD-FDD kwa kuiba kura hali iliyosababisha ushindi kwa chama tawala kinachoongozwa na Rais Pierre Nkurunziza.

No comments:

Post a Comment