Thursday, 28 May 2015
BURUNDI YAKUMBWA NA NJAA...>>!
HALI ya njaa imeikumba Burundi hasa katika mji mkuu wa Bujumbura baada ya wasafirishaji wa mazao kusimamisha huduma yao kuhofia usalama wao.
Kutokana na hali hiyo Serikali imekuwa ikihaha kuwaomba wananchi hasa waliokimbia wa mikoa ya milimani ya Makamba na Ngozi kurejea nchini humo waendelee na kilimo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, mkazi wa Bujumbura ambaye jina lake linahitafadhiwa kwa sababu za usalama, alisema kwa wiki moja sasa huduma muhimu za vyakula zimekuwa adimu nchini humo.
“Hali imekuwa ni mbaya na sasa nchi inakabiliwa na njaa na hatujui la kufanya, fedha zipo lakini bidhaa hakuna hasa chakula, yakiwamo mahindi na mchele.
“Awali tulikuwa tukipata chakula bila tatizo nchi ilipokuwa imetulia lakini tangu yalipoingia machafuko ya kupinga hatua ya Nkurunziza (Pierre, Rais) kuwania urais kwa muhula wa tatu, tunaoana nchi ilipofika sasa,” alisema mkazi huyo wa Bujumbura.
Juzi, Rais Nkurunziza alifanya ziara ya kushtukiza katika mpaka wa Kagunga nchini Tanzania na Burundi na kuwataka warundi wasiikimbie nchi yao akisema kwa sasa ina amani.
Pia aliwataka wananchi kuchangia gharama za kuendesha uchaguzi wa nchi hiyo baada ya wahisani kusimamisha misaada yao kwa Burundi.
Nchi hiyo imekumbwa na machafuko kwa wiki kadhaa sasa ambako waandamanaji wakiwa wakipambana na polisi wakipinga hatua ya Nkurunziza kutaka kugombea urais kwa muhula wa tatu.
Wanasema kitendo hicho ni kukiuka katika ya nchi hiyo inayotamka mtu atagombea urais kwa vipindi viwili tu.
Lakini Nkurunziza na chama chake cha CNDD-FDD amekuwa akidai kwamba hicho kitakuwa kipindi chake cha pili kuchaguliwa na wananchi kwa sababu katika muhula wa kwanza alichanguliwa na Bunge.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment