MWENYEKITI Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi ameitaka
Serikali kuacha kuwashusha thamani vijana kuwa hawawezi kufanya jambo
lolote.
Alisema badala yake itekeleze sera ya uwezeshaji kwa vitendo kama njia ya kuwakwamua katika lindi la umaskini.
Mengi alikuwa akizindua mradi wa ‘Airtel Fursa’ Dar es Salaam jana,
ambao unaendeshwa na kampuni ya mawasiliano ya Airtel Tanzania
kuwasaidia vijana kukuza na kuanzisha biashara.
Alisema vijana wengi wamekuwa hawajiamini tatizo ambalo ni kubwa kwa
Watanzania wote kutokana na mfumo uliowekwa na viongozi wa Serikali kwa
ujumla.
“Serikali ilianzisha sera ya uwezeshaji kwa vijana lakini cha kushangaza
tangu mwaka 2004 hadi sasa hakuna chochote kilichotendeka, viongozi hao
hao wamewaweka vijana namba mbili badala ya kuwa kuwaweka namba moja.
“Ni jambo la kushangaza kuona viongozi haohao badala ya kuwasaidia
vijana wawe namba moja wanabakia kuwaweka namba mbili kwa kusema ‘hamna
uthubutu wala hamna fedha’.
“Nataka kila kijana badala ya kusema nataka kuwa tajiri kama Mengi,
aseme nataka kuwa tajiri zaidi ya Mengi, pia badala ya kusema siwezi, au
haiwezekani, aseme naweza, na inawezekana. Hii ndiyo mbinu ya
mafanikio,” alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Airtel, Balozi Juma Mwapachu, aliwataka vijana
kuchangamkia fursa zinazotolewa na kampuni hiyo ili kujikwamua na
umaskini.
Alisema vijana sasa wanapaswa kutazama kwa mapana na kuona fursa ambazo
zinaweza kuwasukuma katika maendeleo badala ya kusubiri kuletewa kila
kitu na serikali.
Mkurugenzi Mkuu wa Airtel, Sunil Colaso, alisema mradi huo wa fursa una
lengo la kuwanufaisha vijana wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 24.
No comments:
Post a Comment