RAIS Jakaya Kikwete amesema Serikali inafanya mazungumzo na Ofisi ya
Spika wa Bunge kuongeza siku 10 za kuwasilisha miswada mbalimbali.
Kauli hiyo aliitoa juzi mkoani hapa alipofungua Mkutano Mkuu wa Chama
cha Walimu Tanzania (CWT) ambao ulikuwa pamoja na uchaguzi wa nafasi za
juu za chama hicho.
Akizungumza katika mkutano huo ulikuwa na wajumbe zaidi ya 1,200 ambako
mke wake Salma Kikwete pia alihudhuria, Rais Kikwete alitumia fursa hiyo
kuwaaga walimu hao.
Katika hotuba yake iliyojibu zaidi maombi ya walimu, Rais Kikwete
aliwaambia Serikali inaendelea na mazungumzo ya kuongeza siku ili
kuwasilisha bungeni Muswada wa kuanzisha Bodi ya Taifa ya Taaluma za
Walimu (National Teachers Professional Board).
“Tunaendelea na mazungumzo na Ofisi ya Spika tuweze kuongeza siku 10
bungeni zitakazokuwa kwa ajili ya miswada,” alisema Rais Kikwete na
kuongeza:
“Siku hizi tumepanga na Spika kwamba Serikali ndiyo itakayozigharamia.
Na tutakubaliana kabisa muswada wa kwanza uwe wa kuanzishwa Bodi ya
Taifa ya Taaluma za Walimu,” alisema.
Huku wakimuita shemeji, shemeji, Rais Kikwete aliwaeleza kuwa Serikali
ilikwisha kupeleka bungeni Muswada wa Sheria ya kuanzisha Tume ya
Utumishi wa Walimu (Teachers Service Commission) na ulikwisha kusomwa
kwa mara ya kwanza.
“Ninawapenda, nimewapenda na nitaendelea kuwapenda Shemeji zangu. Kwa
sababu natambua mambo yaliyowasilishwa ni ya msingi yanahitaji kufanyiwa
kazi,” alisema Rais Kikwete
Awali akisoma risala ya walimu hao, Katibu Mkuu wa CWT Alhaj Yahaya
Msulwa, alimuomba Rais Kikwete kabla ya kuondoka asaini kuwa sheria,
Muswada wa kuanzisha Tume ya Utumishi wa Walimu (Teachers Service
Commission).
Alhaji Msulwa alimueleza Rais Kikwete matatizo sugu yanayowakili walimu
nchini kwa miaka mingi ambayo ni uhaba wa walimu hasa wa sayansi, madeni
ya walimu na posho ya kufundishia.
No comments:
Post a Comment