BAADHI ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC),
wameelezea kufurahishwa na hotuba iliyotolewa na Mwenyekiti wa chama
hicho, Rais Jakaya Kikwete.
Akifungua mkutano wa Halmashauri Kuu mjini hapa juzi, Rais Kikwete
alisema salama ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu,
ni kuteua wagombea wazuri wanaokubalika kwa wananchi.
Rais Kikwete aliwaagiza viongozi wa chama hicho kuzingatia sifa na
vigezo na mwisho wa siku kuteua wagombea wazuri katika ngazi zote za
urais, ubunge na udiwani ili chama hicho kiweze kushinda bila jasho.
Wakizungumza na MTANZANIA nje ya ukumbi wa jengo la makao makuu ya chama
hicho (White House), wajumbe hao walisema hotuba ya Rais Kikwete imetoa
dira kwa chama hicho kuelekea katika uchaguzi.
Wajumbe hao walisema, hotuba ya Rais Kikwete imesimama katika uhalisia na kwamba hakuonesha mwelekeo iwapo ana mgombea wake.
Mjumbe wa Wilaya ya Musoma, Vedastus Mathayo, alisema hotuba hiyo imetoa
mwelekeo kwa chama hicho na njia madhubuti kuelekea katika uchaguzi.
“Nimefurahishwa na hotuba yake, hasa pale aliposema chama kiteue mtu
anayekubalika na wananchi. Tuchague mtu anayetakiwa na watu si
tunayemtaka sisi viongozi.
“Utaratibu wa kuteua mtu asiyekuwa na uwezo wa kutosheleza kiu ya wananchi halafu anabebwa na chama sasa no (hapana).
“Tunahitaji ateuliwe mtu aggressive (makini) atakayekibeba chama na
kukiletea ushindi, si chama kimbebe mtu, zama hizo hivi sasa hazipo,”
alisema.
Balozi Karume
Mjumbe wa NEC kutoka Zanzibar, Balozi Alli Karume, alisema
amefurahishwa na hotuba hiyo, kwani Rais ameonesha ukomavu wake katika
medani ya siasa ndani ya chama hicho.
Balozi Karume alisema hotuba ya Rais Kikwete itatumika kukivusha
chama hicho katika uchaguzi mkuu mwaka huu na uchaguzi mwingine na
kuongeza anaamini hata nukuu zake zitakuwa dira ya kukiongoza chama
hicho kwa siku za mbele.
Balozi Karume alisema kwa hotuba hiyo ni wazi kuwa Rais Kikwete
amezungumzia mambo ya msingi na amedhihirisha anatanguliza maslahi ya
chama chake na si marafiki zake.
“Ameweka wazi kwenye suala la kuchagua kiongozi kwa ajili ya kupeperusha
bendera ya chama, hakuna sababu ya kutanguliza urafiki,” alisema.
Amenukuu baadhi ya maneno yaliyokuwa yakizungumzwa na Rais wa Awamu
ya Kwanza, Mwalimu Julius
Nyerere, lakini naamini hata hotuba yake ya
leo (jana) itakumbukwa na kizazi cha sasa na kijacho.
“Hotuba hii ya Rais itatumika kama nukuu kwa ajili ya chaguzi na
namna ya kukiendesha chama. Nimekaa nje ya nchi kwa muda mrefu,
alichozungumza mwenyekiti amedhihirisha kiwango chake kwenye siasa ni
cha hali ya juu,” alisema.
Alisema Rais Kikwete amezungumza na wajumbe wa NEC, lakini hakuonesha
anataka nani achaguliwe, kwani hakuwa upande wowote zaidi ya kuzungumza
hali halisi ya chama hicho na wakati uliopo.
“Ingekuwa wengine hapa tungeanza kupata maelekezo ya rais kuhusu nani
anataka awe rais ajaye baada ya kumaliza muda wake, lakini yeye hana
chaguo lake, hivyo ametaka sifa, kanuni na maadili ya chama iwe dira ya
kupata viongozi,” alisema.
Raya
Mjumbe mwingine kutoka Wilaya ya Rorya, mkoani Mara, Thobias Raya,
alisema hotuba hiyo imetoa suluhisho la ushindi wa CCM katika uchaguzi
ujao.
Alisema kwa mazingira ya sasa, kinachoangaliwa ni uwezo wa mtu na
kukubalika kwake na si suala la fedha kama baadhi ya watu wanavyodhani.
“Fedha si msingi wa kumpata mgombea. Chama kinahitaji kuteua mgombea
mzuri atakayekivusha chama kwa nafasi anayoomba bila kujali hali ya
kiuchumi,” alisema.
Kimbita
Naye Mjumbe kutoka Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Fuya Kimbita,
alisema hotuba ya Rais Kikwete ni darasa tosha kwa chama na kwamba kila
mjumbe anapaswa kutembea na hotuba hiyo.
“Kwa kweli ni hotuba nzuri sana, binafsi nimefurahishwa, amezungumzia
hali halisi ya siasa ya Tanzania kwa hivi sasa, amewafungua macho
wajumbe.
“Wakati wenzetu wanaishi kwa kuzingatia fikra na hisia na kizazi cha
sasa, sisi tunaishi na kizazi cha sasa lakini mipango na utaratibu wetu
tunafanya kizamani, lazima tubadilike,” alisema.
Bulembo
Akizungumzia hotuba ya Rais Kikwete, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi
Taifa, Alhaj Abdallah Bulembo, alisema amefurahishwa na hotuba hiyo,
lakini naye alitumia nafasi hiyo kuweka wazi mgombea wa CCM lazima awe
msafi asiyekuwa na kashfa chafu.
Alisema kuwa mgombea wa CCM anayetaka kugombea uongozi si yule mwenye
mbwembwe na madoido mengi, bali ni mtu mwenye kujitambua. “Anayejiamini
yeye ni msafi agombee, lakini kama ni mchafu ni vema akakaa kando,”
alisema.
Mgeja
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja,
alisema hotuba ya Rais Kikwete ni darasa tosha kwa wana-CCM, hasa
kipindi hiki, kwani kwenye suala la kuchagua viongozi, ameeleza wazi
umuhimu wa kuchagua viongozi kulingana na kukubalika kwao kwa wananchi.
Aliwataka wajumbe wa NEC na wana CCM kwa ujumla kuisikiliza kwa
umakini hotuba hiyo ili kufahamu misingi ya chama hicho, huku akielezea
kuunga mkono kauli ya Rais kuwa lazima wanachama hao wasome alama za
nyakati kwa kuchagua viongozi wazuri.
“Nimesikiliza vizuri hotuba ya mwenyekiti wetu, amezungumza mambo ya
msingi ambayo kwetu sisi ni darasa tosha. Lazima tusome alama za
nyakati.
“Uchaguzi wa Sekali za mitaa uliofanyika mwaka jana tumeshuhudia baadhi
ya mitaa imekwenda upinzani kwasababu ya viongozi kuwa na watu wao na si
wale wanaotakiwa na wananchi.
“Hivyo lazima tuchague viongozi kwa kuangalia wananchi wanamtaka nani na si kiongozi anataka nani awe kiongozi,” alisema Mgeja.
No comments:
Post a Comment