Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema matamanio ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya kuwaletea Watanzania mabadiliko waliyoyakosa ndani ya CCM yanaenda kutimia katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Mbowe aliyasema hayo jana katika mkutano wa chama
wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe
jijini Dar es Salaam ambako pamoja na mambo mengine alizindua kitabu cha
mambo aliyoyafanya mbunge wa jimbo hilo, Halima Mdee na wimbo maalumu
wa msanii wa nyimbo za Injili, Flora Mbasha.
Akizungumza katika mkutano huo uliorushwa moja kwa
moja na ITV, Mbowe alisema katika maeneo yote ya nchi, watu wamekata
tamaa ya maisha kutokana na uongozi mbaya wa chama tawala, hivyo wako
tayari kufanya mabadiliko ya mfumo wa utawala.
“Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu matamanio ya
Mwalimu Nyerere yanaenda kutimia. Watanzania wanataka mabadiliko ambayo
wameyakosa ndani ya CCM. Nimezunguka nchi nzima na kubaini kuwa wananchi
wanazo sababu na uwezo wa kuyaleta mabadiliko kutokana na kiu
waliyonayo,” alisema.
Mbowe aliyeanza mkutano huo kwa kukagua gwaride la
kikundi cha Red Brigade, alitoa kauli hiyo akimnukuu Mwalimu Nyerere
aliyepata kusema kuwa, “Watanzania wanataka mabadiliko. Wasipoyapata
ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM.”
“Nimepokea malalamiko kutoka kwa askari mstaafu wa Jeshi la
Wananchi (JWTZ) ambaye analipwa Sh22,000 kwa mwezi. Anaamini Chadema
itamtendea haki ili kipato chake kiweze kukidhi mahitaji,” alisema
Marando.
Mkutano huo pia ulizindua kikosi cha Red Brigade
ambao wapo 200 katika kila jimbo nchini, wakiwa na jukumu la kulinda
kura katika vituo vyote kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Gwajima ahutubia
Katika mkutano huo, Askofu Josephat Gwajima wa
Kanisa la Ufufuo na Uzima, mwimbaji Flora Mbasha pamoja na mumewe
Emmanuel Mbasha ni miongoni mwa wageni walioalikwa katika mkutano huo.
Baada ya Mbowe kuhutubia, mashabiki walipiga kelele wakitaka Askofu Gwajima naye ahutubie.
Askofu huyo alipopewa nafasi alisema kiongozi
anapokaribia kupoteza madaraka Mungu humpa ukichaa na kuacha kuona
matatizo ya watu.
“Kwa hali ilivyo sasa, viongozi wa Serikali
wamepewa ukichaa, hawanaoni matatizo ya watu. Muda wa mabadiliko ndio
umewadia, alisema.
Bavicha watishia
Awali, Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha)
lilieleza dhamira ya kufanya maandamano kuishinikiza NEC kama
haitaongeza muda wa kuandikisha wapigakura.
Katibu Mkuu wa Bavicha Taifa, Julius Mwita
alieleza hayo wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa
kata wa chama hicho katika Jimbo la Ukonga, Dar es Salaam.
“Kwa mijibu wa ratiba ya Tume, uandikishaji
utafanyika kuanzia Julai 4 mpaka 16. Dar ina wakazi zaidi ya milioni
nne, je, muda huo unatosha kuwafikia watu wote wanaostahili
kuandikishwa? Kama hautoshi basi tuishinikize Tume kuongeza muda huo,”
alisema Mwita.
Aliongeza endapo hilo halitafanywa Bavicha itaandaa maandamano ili kuishinikiza watu wote wenye sifa waaandikishwe.
Alitumia fursa hiyo kuzungumzia mchakato wa
uandikishaji wapigakura kuwa unahitaji kutazamwa kwa namna nyingine ili
kuwatendea haki wananchi ambao wana shauku ya kutimiza haki hiyon ya
kikatiba.
“Juzi nilikuwa Mbeya, nimeshuhudia wananchi
wakilala katika vituo vya kuandikishia kutokana na hofu waliyonayo
kukosa uchaguzi mkuu. Namkumbusha Jaji Lubuva (Damian, mwenyekiti wa
Tume ya uchaguzi) aongeze muda na isiwe siku saba kama ilivyopangwa
awali. Kutofanya hivyo atakuwa anajitafutia lawama ambazo hakutakuwa na
kiongozi yeyote wa CCM atakayesimama kumtetea pindi wananchi
watakapokuwa wanamlaumu hapo baadaye,” alisema.
Mwenyekiti huyo mwenza wa umoja wa Katiba ya
wananchi (Ukawa), pia alibainisha mkakati wa umoja huo kugomea na
kuipinga rasimu inayotaka vyombo vyote vya habari kujiunga na Shirika la
Habari Tanzania (TBC) kwa taarifa ya habari ya saa 2.00 usiku.
“Tutaleta vurugu. Tutasimamisha Bunge kupinga
sheria hiyo kwa sababu hiyo ni hujuma ambayo wananchi hawaikubali na
mimi kama kiongozi wa upinzani nitalisimamia hilo,” alieleza.
Akimakaribisha Mbowe, Naibu Katibu Mkuu na Mbunge
wa Ubungo, John Mnyika alisema mkutano huo ni muhimu na chama
kimeuandaaa ili kuthamini umuhimu wa wanawake katika jamii.
“Mwenyekiti fikiria kama wewe unabeba mimba miezi
tisa, ujifungue na kumlea mtoto. Hayo ndiyo wanayoyafanya wanawake hawa.
Ni lazima tukubali ujasiri wao kwa kuyajali majukumu yao,” alisema
Mnyika.
Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani, Mabere
Marando alisema Chadema kimejipanga kuwaleta viongozi wake wote jijini
hapa kufanya kampeni ya uandikishaji katika daftari la kudumu ili
wapigakura wafike milioni 3.5 na kuiondoa CCM madarakani.
No comments:
Post a Comment