KIWANGO kibovu kilichoonyeshwa na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kwenye mchezo wa kwanza wa michuano ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika (Cosafa) dhidi ya Swaziland kimekera Watanzania wengi, hasa baada ya kupoteza kwa kufungwa bao 1-0.
Bao hilo pekee la Swaziland lilifungwa na beki wa kulia, Simbizo Mabila, aliyewahadaa mabeki wa Stars na kupiga shuti lililomshinda kipa, Deogratius Munishi ‘Dida’.
Matokeo hayo yamewaumiza Watanzania wengi nchini, ambapo mara baada ya kumalizika mechi hiyo kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, watu wengi wamelaumu kiwango kibovu kilichoonyeshwa na Stars.
“Siku zote kila mtu anavuna alichopanda, Taifa Stars wamevuna walichopanda, timu inachaguliwa kwa upendeleo, wachezaji waliofanya vizuri na wenye uwezo hawachaguliwi ukiuliza au ukiongea wanasema kocha anajua tumwachie, hebu tujiulize huyu kocha ana uchungu kweli na kipigo anachopata kuliko sisi Watanzania?” alihoji Charles Mayilla kupitia mtandao wa facebook.
Stars iliyopo Kundi B itateremka tena dimbani leo kuvaana na Madagascar, iliyotoka kuifunga Lesotho mabao 2-1 kwenye mechi ya ufunguzi, mchezo huo utafanyika Uwanja wa Moruleng nchini Afrika Kusini kuanzia saa 12.00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Kipigo hicho kinakuja wiki chache mara baada ya wapenzi wengi wa soka nchini kulalamikia uteuzi wa kikosi wa Kocha Mkuu, Mart Nooij, ambaye ameendelea kuwaita baadhi ya wachezaji wanaokaa benchi kwenye timu zao huku akiwaacha wale waliofanya vizuri.
Baadhi ya wachezaji aliosafiri nao na wamekuwa wakiwekwa benchi kwenye mechi nyingi za timu zao msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) ni kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ (Yanga), Mwadini Ally (Azam), Hassan Dilunga (Yanga) na John Booco (Azam), aliyesumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.
Stars ilianza kucheza mchezo kwa kasi nzuri dhidi ya Swaziland, lakini kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda kuanzia dakika ya 30 wachezaji walionekana kucheza kwa kutoelewana hasa idara ya kiungo iliyokuwa ikiundwa na Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto na Erasto Nyoni, huku pia eneo la ushambuliaji likipwaya ambalo lilikuwa na Bocco, Mrisho Ngassa na Simon Msuva.
Swaziland iliyokuwa ikionekana kucheza kitimu kila ilipomiliki mpira, iliweza kutumia mwanya huo na kupata bao, ambalo liliwapoteza kabisa wachezaji wa Stars, ambao walitoka mchezoni na kila mchezaji kucheza kivyake, jambo ambalo halikuwa msaada kwa timu na matokeo kubaki kama yalivyo.
Makocha wanena
Akizungumza na MTANZANIA kocha mkongwe visiwani Zanzibar, Hemed Morocco, anayeinoa timu ya taifa ya huko ‘Zanzibar Heroes’, alisema hakuna njia ya mkato ya mafanikio kwa Stars, amedai lazima iachane na wachezaji wazee na kutengeneza kikosi bora cha vijana.
“Kila siku matokeo yetu yamekuwa ni kufungwa, mimi naona bado tunakurupuka, tunakumbatia timu ile ile ya wazee, Tanzania ina wachezaji wengi vijana waliobarikiwa vipaji, tukitaka kufika mbali tutengeneze kikosi bora cha vijana wenye umri wa miaka 17 ambacho baada ya miaka minne kitatupa mafanikio,” alisema.
Naye kocha mzoefu nchini, Kennedy Mwaisabula, alisema matokeo ya Stars dhidi ya Swaziland yametokana na kupwaya eneo la ushambuliaji waliopoteza nafasi kadhaa za wazi, huku akipata shaka kwenye safari ya timu hiyo kufuzu Mataifa ya Afrika (AFCON) 2017 na Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).
“Uteuzi wa kikosi ndio unaiangusha timu, si vibaya kocha kuita kikosi chenye sura zile zile, lakini lazima tuangalie ya kuwa kikosi anachoendelea kukiita kina mafanikio, kama hakina mafanikio kocha lazima abadili kikosi na kujaribu wachezaji wengine, tunaona hapo amewaacha wachezaji bora kwenye ligi kama mshambuliaji Mandawa (Rashid), Malimi Busungu yule wa Mgambo, full back Kessy (Hassan),” alisema.
Alisema ipo haja kwa kocha wa Stars, Nooij kupata usaidizi mzuri wa ushauri kwa makocha wazawa ambao wanawajua vizuri wachezaji wa hapa, huku pia akieleza lazima Mholanzi huyo awe na mahusiano mazuri na makocha wa timu za Ligi Kuu.
“Kuna makocha wakongwe kabisa nchini kama mzee Kibadeni (Abdallah) na Mshindo Msolla, lazima watumiwe kwenye ushauri kwani wameipatia nchi mafanikio, kingine kocha inaonekana hana mahusiano mazuri na makocha wa ligi, kwani hata uteuzi wake amekuwa akiita wachezaji wagonjwa, hivyo lazima aimarishe mahusiano kwani wachezaji wanatoka kwenye klabu,” alisema.
Hatima ya Stars Cosafa
Mpaka sasa kinara wa Kundi B ni Madagascar yenye pointi tatu sawa na Swaziland, Lesotho na Stars zote hazina pointi.
Hivyo lazima Stars iifunge Madagascar leo na pia iinyuke Lesotho kwenye mchezo wa mwisho keshokutwa, ili kufufua matumaini ya kufuzu kwa robo fainali ya michuano hiyo, kinara wa kundi hilo atakutana na timu mwalikwa Ghana, iliyofuzu moja kwa moja hatua hiyo.
Stars bado ina mtihani mkubwa mwezi ujao itakapoanza kuchanga karata za kufuzu Chan mwakani, imepangwa kucheza na Uganda ‘The Cranes’ kwenye hatua ya awali, huku katika ile ya AFCON ikiwekwa Kundi G sambamba na vigogo Misri, Nigeria pamoja na Chad inayoonekana kuwa kibonde
No comments:
Post a Comment