POLISI wilayani Bunda, mkoani Mara, wanadaiwa kugoma kuchangia fedha za
mafuta kwa ajili ya kusafirisha mwili wa askari mwenzao, Koplo Mahamudu
Magasa, aliyefariki dunia baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa malaria kwa
muda mfupi.
Mafuta hayo yalikuwa yanatakiwa kwa ajili ya kusafirisha mwili wa Koplo
Mahamudu kwenda nyumbani kwako, Wilaya ya Mahenge, mkoani Morogoro.
MTANZANIA jana ilifika Kituo Kikuu cha Polisi cha Wilaya ya Bunda na
kukuta umati mkubwa wa askari polisi wakiwa kituoni hapo, wakipinga
hatua ya kulazimishwa kuchangia mafuta kwa vile si jukumu lao.
Walisema kuwa kitendo hicho kinaonyesha wazi kwamba Serikali haithamini
utumishi wao, kwani watumishi wa idara nyingine wanapofariki dunia fedha
hutolewa na Serikali kwa ajili ya kusafirisha miili yao.
“Leo (jana) kafariki dunia mwenzetu imekuwa hivi, je, kama angekuwa mke
wake au mtoto ingekuwaje, si ndiyo aibu kabisa,” alisema askari mmoa
ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Walisema siku zote wamekuwa wamejiwekea utaratibu endapo mwenzao
anafariki dunia huchangia Sh 5,000 kila mmoja, ili ziweze kusaidia
familia ya marehemu na si kuchangia mafuta ya kusafirisha.
Hata hivyo, wakati polisi hao wakiwa wamekusanyika nje ya kituo hicho
wakipinga hatua hiyo, maofisa wa jeshi hilo wilayani hapa wakiongozwa na
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bunda (OCD) Gwisael, walikuwa kwenye kikao cha
pamoja.
Gazeti hili lilipata nafasi ya kuzungumza na OCD Gwisael, ambaye alikanusha madai ya askari hao kuchangishwa fedha za mafuta.
Alisema askari hutoa mchango wa Sh 5,000 kwa hiari yao kama ilivyo
kawaida na siyo za mafuta ya Sh 10,000 kama inavyodaiwa na baadhi ya
askari.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Philipo Kalangi,
akizungumzia tukio hilo alisema ofisi yake imetoa gari na lita 220 za
mafuta kwa ajili ya kusafirisha mwili wa Koplo Magasa.
Alisema ni marufuku kwa askari yeyote kuchangishwa mchango wa mafuta.
“Tayari nimeshatoa gari na mafuta lita 220 kwa ajili ya kusafirisha
mwili wa askari wangu… pia tunatoa na posho ya kujikimu kwa askari
watakaosafirisha mwili wa marehemu, nani kawaambia wachangie tena…sisi
tuna utaratibu wetu wa Serikali, siyo kuchangisha askari fedha za
mafuta,” alisema Kamanda Kalangi
Gazeti hili jana saa 7:52 mchana lilishuhudia gari la polisi lililotumwa
na Kamanda Kalangi kutoka mjini Musoma, lenye namba za usajili DFP
1822, likiwa Kituo cha Polisi Bunda kwa ajili ya kuanza safari ya kwenda
Mahenge.
No comments:
Post a Comment