Ligi Kuu ya England imemalizika kwa mtindo wa aina yake, baadhi ya
timu zikitoka na karamu ya mabao na nyingine zikiweka rekodi mbaya.
Hull
wameshuka daraja baada ya Newcastle waliokuwa wakiviziana nani ashuke
kuwafunga West Ham huku Hull wenyewe wakienda suluhu na Manchester
United. Hull walihitaji ushindi lakini pia wakiomba Newcastle ama
wafungwe au watoshane nguvu na wapinzani wao.
Kocha Steve Bruce
ameeleza kusikitishwa kwake na kushuka daraja, akisema vijana wake
hawakucheza vyema. Mchezaji wa zamani wa Tottenham Hotspur aliyejiunga
Hull kwa mkataba wa miaka mitatu, Michael Dawson amesema hakutarajia
kitu kama hicho alipokuwa akisaini mkataba.
Arsenal walimaliza
ligi kwa nguvu na kushika nafasi ya tatu hivyo kufuzu moja kwa moja kwa
hatua za makundi za Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), baada ya kuwakandika
West Bromwich Albion 4-1.
Mabao ya Arsenal yalifungwa na Theo Walcott matatu na Jack Wilshere moja. West Brom walifunga kupitia kwa Gareth McAuley.
Walcott alichezeshwa kama mshambuliaji wa kati, nafasi ambayo amekuwa
akisema anaipenda, lakini huwa hapangwi kutokana na kuwapo wengine
waliobobea hapo kama Olovier Giroud.
Walcott bado hajafikia
mwafaka na klabu yake juu ya kuhuisha mkataba wake akiwa amebakiza
karibu mwaka mmoja tu umalizike. Arsenal hawajapata kufungwa kwenye
mechi ya mwisho wa msimu tangu 2005 walipolazwa 2-1 na Birmingham.
Mahasimu
wa Arsenal wa London Kaskazini, Spurs wamefanikiwa kuwavuka Liverpool
na kufuzu moja kwa moja kwa hatua ya makundi ya Ligi ya Europa, baada ya
kuwafunga Everton 1-0 kwa bao la mshambuliaji machachari chipukizi wa
England, Harry Kane.
Spurs wamewazidi Liverpool kwa pointi mbili
baada ya Liver kukung’utwa mabao 6-1 kwenye mechi ya mwisho ambayo
ilikuwa pia ya kumuaga nahodha wao, Steven Gerrard anayekwenda kucheza
soka nchini Marekani.
Ushindi
wa Spurs umewaweka Everton katika rekodi mbaya, wakiwa wamemaliza ligi
chini ya timu 10 za juu kwa mara ya kwanza tangu 2006. Msimu huu Everton
walianza ligi kwa kusuasua, tofauti na msimu uliopita ambapo vijana hao
wa Roberto Martinez walikuwa wazuri. Huu ulikuwa mchezo wa tatu
kupoteza miongoni mwa minne iliyopita.
Kwa upande wa Liverpool,
hii ni mara ya kwanza katika miaka 52 kuruhusu mabao sita kwenye mechi
moja, ambapo kocha Brendan Rodgers naye ameweka rekodi mbaya ya kukosa
walau kikombe kimoja katika misimu mitatu.
Rodgers amekiri kwamba
yupo katika shinikizo kubwa na atakubali kuondoka iwapo wenye klabu
wataamua hivyo, japokuwa anasema pia kwamba bado ana mengi ya kuwasaidia
kama atabaki Anfield.
Liver ambao msimu uliopita nusura watwae
ubingwa kama si kuvurunda mechi za mwisho na kupitwa na Manchester City,
wamemaliza katika nafasi ya sita hivyo watatakiwa kuanzia raundi ya
tatu ya kufuzu kwa Ligi ya Europa Julai 30, ambapo wakifuzu watakuwa na
mechi nyingi katika msimu ujao ambazo pia huchosha.
Southampton
ndio wanaowafuata Liverpool katika nafasi ya saba ambapo Jumapili hii
walikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Man City ambao wamemaliza
ligi wakiwa nafasi ya pili, baada ya kuvuliwa ubingwa na Chelsea mapema.
Swansea
waliokuwa wazuri nao wamemaliza ligi vibaya kwa kufungwa 1-0 na Crystal
Palace. Hata hivyo wamebaki kwenye nafasi ya nane waliyokuwa
wakishikilia , wakifuatiwa na Stoke huku Palace wakikamata nafasi ya 10.
Palace
wameimarishwa na kocha wao Alan Pardew aliyeajiriwa kutoka Newcastle
wakati timu ikiwa katika eneo la hatari la kushuka daraja, na sasa
amewawekea msingi mzuri kwa msimu ujao.
Matokeo ya mechi za mwisho
wa EPL Jumapili hii yalikuwa Arsenal kuwalaza West Brom 4-1, Aston
Villa kulala 1-0 kwa Burnley waliokwishashuka daraja; Chelsea kuwafunga
Sunderland 3-1; Palace wakawapiga Swansea 1-0 na Everton kulala 1-0
kwaSpurs.
Kwingineko Hull na Man United walikwenda suluhu;
Leicester wakawakung’uta QPR waliokwishashuka daraja mapema 5-1; Man
City wakawapiga Southampton 2-0, Newcastle wakawazidi nguvu West Ham kwa
2-0 na Stoke kuwaadhibu Liverpool 6-1.
Kwa hali hii timu
zilzioshuka daraja ni Hull waliomaliza wakiwa na pointi 35, Burnley
wenye 33 na QPR mkiani na 30. Aston Villa ndio walibaki wakichungulia
kushuka lakini wakishajihakikishia kabla kutoshuka kwani pointi zao 30
zilikuwa zinawatosha kubaki juu.
Pointi hizo ni sawa na walizokuwa
nazo Sunderland ambao wameokolewa kushuka daraja na Dick Advocaat
aliyeajiriwa kwa muda kwa ajili hiyo na sasa amerudi kwao Uholanzi
kumuomba mkewe ruhusa ya kuendelea na klabu hiyo msimu ujao.
Newcastle
walikuwa katika wakati mgumu na wangeweza pia kushuka kama si
kujitahidi jana na pia kusaidiwa na matokeo ya Hull kutoshinda, wakiwa
katika mkwaruzano baina ya washabiki na mmiliki Mike Ashley lakini pia
kocha John Carver akiwa haelewani vya kutosha na wachezaji wake.
Timu
zilizokuwa na uhakika wa kubaki EPL kwa zaidi ya wiki moja hivi ni
Leicester, West Brom, West Ham na Everton lakini zikiwa hazina fursa ya
kucheza michuano ya Ulaya. Jumatatu hii Norwich wanacheza na
Middlesbrough kujua nani atapanda EPL kuungana na Bournemouth na
Watford.
No comments:
Post a Comment